8
Kwa kiongozi wa muziki; weka kwenye mtindo wa gittith. Zaburi ya Daudi.
1 Yahweh Bwana wetu, ni jinsi gani jina lako ni tukufu katika dunia yote, wewe ufunuaye utukufu wako juu mbinguni.
2 Kutoka katika midomo ya watoto na vichanga umeumba sifa kwa sababu ya utukufu wako, ili kuwanyamazisha maadui wote na walipa kisasi wote.
3 Ninapozitazama mbingu, ambazo vidole vyako vimeumba, mwezi na nyota, ambazo umeziweka kila mmoja katika nafasi yake,
4 Binadamu ni nani hata umtazame, na watu hata uwajali wao?
5 Umewaumba chini kidogo kuliko viumbe vya mbinguni na umewazunguka na utukufu na heshima.
6 Umemfanya binadamu kutawala kazi ya mikono yako; umeviweka vitu vyote chini ya miguu yake:
7 kondoo na ng'ombe wote, na hata wanyama wa porini,
8 ndege wa angani, na samaki wa baharini, na vyote vipitavyo katika mikondo ya bahari.
9 Yahweh Bwana wetu, ni jinsi gani jina lako ni tukufu katika dunia yote!