88
Wimbo, Zaburi ya wana wa Kora; kwa kiongozi wa muziki; seti kwenye mtindo wa Mahalath Leannoth. Zaburi ya Heman mu Ezrahite.
1 Yahwe, Mungu wa wokovu wangu, ninalia mchana na usiku mbele zako.
2 Sikiliza maombi yangu; utazame kulia kwangu.
3 Maana nimejawa taabu, na uhai wangu umefika kuzimuni.
4 Watu hunichukulia kama wale waendao chini shimoni; mimi ni mtu asiye na nguvu.
5 Nimetelekezwa miongoni mwa wafu; niko kama mfu alalaye katika kaburi, wao ambao wewe huwajari tena kwa sababu wametengwa mbali na nguvu zako.
6 Wewe umeniweka katika sehemu ya chini kabisa ya shimo, sehemu yenye giza na kilindini.
7 Gadhabu yako yanielemea, na mawimbi yako yote yanatua juu yangu. Selah
8 Kwa sababu yako, wale wanijuao wote hunikwepa. Umenifanya wakutisha machoni pao. Nimefungwa na siwezi kutoroka.
9 Macho yangu yamefifia kutokana na shida; kila siku nakuita wewe, Yahwe; ninakunyoshea wewe mikono yangu.
10 Je! utafanya miujiza kwa ajili ya wafu? Wale waliokufa watafufuka na kukusifu wewe? Selah
11 Uaminifu wa agano lako utatangazwa kaburini? au uaminifu wako mahali pa wafu?
12 Matendo yako ya ajabu yatajulikana gizani? au haki yako katika mahali pa usahaulifu?
13 Lakini ninakulilia wewe, Yahwe; wakati wa asubuhi maombi yangu huja kwako.
14 Yahwe, kwa nini unanikataa? Kwa nini unauficha uso wako mbali nami?
15 Nimekuwa nikiteswa kila siku na hatihati ya kifo tangu ujana wangu. Nimeteseka dhidi ya hofu yako kuu; ninakata tamaa.
16 Matendo yako ya hasira yamepita juu yangu, na matendo yako ya kutisha yameniangamiza.
17 Siku zote yananizingira mimi kama maji; yote yamenizunguka mimi.
18 Wewe umemuondoa kwangu kila rafiki na anijuaye. Na sasa anijuaye pekee ni giza.