95
1 Oh njoni, tumwimbie Yahwe; na tumwimbie kwa shangwe mwamba wa wokovu wetu.
2 Tuingie uweponi mwake kwa shukrani; tumwimbie yeye kwa zaburi ya sifa.
3 Kwa maana Yahwe ni Mungu mkuu na Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Mkononi mwake zimo bonde za dunia; navyo vilele vya milima ni vyake.
5 Bahari ni yake, maana aliiumba, na mikono yake ilitengeneza nchi kavu.
6 Oh njoni, tumwabudu na tupige magoti; tupige magoti mbele za Yahwe, muumbaji wetu:
7 Kwa maana yeye ni Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho yake na kondoo wa mkono wake. Ni heri leo mngesikia sauti yake!
8 Msiifanye migumu mioyo yenu, kama vile huko Meriba, au kama ile siku ya Masa jangwani,
9 ambako baba zenu walinijaribu na kunipima, japo walikuwa wameyaona matendo yangu.
10 Kwa miaka arobaini nilikasirishwa na kizazi hicho na kusema, 'Hawa ni watu ambao mioyo yao imepotoka; hawazijui njia zangu.'
11 Hivyo katika hasira yangu niliapa kwamba wasingeingia kamwe mahali pa pumziko.”