96
1 Oh, mwimbieni Yahwe wimbo mpya; mwimbieni Yahwe, nchi yote.
2 Mwimbieni Yahwe, tukuzeni jina lake; tangazeni wokovu wake siku hadi siku.
3 Tangazeni utukufu wake kati ya mataifa, matendo yake ya ajabu kati ya mataifa.
4 Maana Yahwe ni mkuu na wakusifiwa sana. Ni wakuhofiwa kuliko miungu mingine.
5 Maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, bali ni Yahwe aliye zifanya mbingu.
6 Heshima na adhama ziko mbele zake. Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.
7 Mpeni Yahwe sifa, enyi ukoo wa watu, mpeni sifa Yahwe kwa ajili ya utukufu wake na nguvu.
8 Mpeni Yahwe utukufu ambao unastahili jina lake. Leteni matoleo na muingie nyuani mwake.
9 Mpigieni magoti Yahwe mkiwa mmevaa mavazi ambayo yanaheshimu utakatifu wake. Nchi yote tetemekeni mbele zake.
10 Semeni kati ya mataifa, Yahwe anatawala.” Ulimwengu pia umeimarishwa; hauwezi kutikiswa. Yeye huwahukumu watu kwa haki.
11 Mbingu na zifurahi, na nchi ishangilie; bahari na ivume na vyote viijazavyo vipige kelele kwa shangwe.
12 Mashamba yashangilie na vyote vilivyomo. Kisha miti ya mstuni ipige kelele kwa furaha
13 mbele za Yahwe, maana yeye anakuja. Anakuja kuihukumu nchi. Naye atauhukumu ulumwengu kwa haki na mataifa kwa uaminifu wake.