99
1 Yahwe anatawala; mataifa na yatetemeke. Ameketi juu ya makerubi; nchi inatetemeka.
2 Yahwe ni mkuu katika Sayuni; naye ametukuka juu ya mataifa yote.
3 Nao walisifu jina lako kuu na lenye kutisha; yeye ni mtakatifu.
4 Mfalme ana nguvu, naye hupenda haki. Wewe umeimarisha haki; umetenda haki na hukumu katika Yakobo.
5 Msifuni Yahwe Mungu wetu na sujuduni miguuni pake. Yeye ni mtakatifu.
6 Musa na Haruni walikuwa miongoni mwa makuhani wake, na Samweli alikuwa miongoni mwa wale walio muomba Yeye. Walimuomba Yahwe, naye akawajibu.
7 Alizungumza nao toka nguzo ya wingu. Walizishika amri zake takatifu na sheria ambazo aliwapatia.
8 Wewe uliwajibu, Yahwe Mungu wetu. Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe, lakini uliye adhibu matendo yao ya dhambi.
9 Msifuni Yahwe Mungu wetu, na mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu, maana Yahwe Mungu wetu ni Mtakatifu.