26
1 Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi akujificha katika vilima vya Hakila, ambavyo viko mbele ya jangwa?”
2 Kisha Sauli akaamka na kwenda chini ya jangwa la Zifu, akiwa na watu elfu tatu waliochaguliwa katika Israeli, wamtafute Daudi katika jangwa la Zifu.
3 Sauli akaweka kambi kwenye kilima cha Hakila, kilicho mbele ya jangwa, kando ya barabara. Lakini Daudi alikuwa akikaa nyikani, na akaona kwamba Sauli alikuwa anamfuatia huko jangwani.
4 Hivyo Daudi akawatuma wapelelezi na akafahamu kwamba hakika Sauli alikuwa amekuja.
5 Daudi akaamka na kwenda hadi mahali ambapo Sauli alipiga kambi; akaona mahali alipolala Sauli, na Abneri mwana wa Neri, mkuu wa jeshi lake; Sauli alilala katikati ya kambi, na watu walipiga kambi kumzunguka, na wote wamesinzia.
6 Ndipo Daudi akamwambia Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, ndugu yake Yoabu, “Ni nani atakwenda nami kambini kwa Sauli? Abishai akasema, “Mimi nitashuka pamoja nawe.”
7 Hivyo Daudi na Abishai wakaliendea jeshi usiku. Na Sauli alikuwapo akisinzia ndani ya kambi, mkuki wake umechomekwa chini pembeni mwa kichwa chake. Abneri na Askari wake wamelala kwa kumzunguka.
8 Kisha Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemweka adui yako mkononi mwako. Basi tafadhali acha nimchome mkuki nimtoboe hadi chini kwa pigo moja. Sitampiga mara mbili.”
9 Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; kwa maana nani awezaye kunyoosha mkono wake dhidi ya mtiwa mafuta wa BWANA na asiwe na hatia?”
10 Daudi akasema, “Kama BWANA aishivyo, BWANA atamuua, au siku ya kufa kwake itakuja, au atakwenda katika vita na ataangamia.
11 BWANA apishe mbali nisinyooshe mkono wangu dhidi ya mtiwa mafuta wake; lakini sasa, nakusihi chukua mkuki uliokichwani pake na jagi la maji, tuondoke.”
12 Hivyo Daudi akachukua mkuki na jagi la maji kutoka kichwani pa Daudi, wakatoweka. Hakuna mtu aliyewaona au kufahamu habari hii, wala hakuna aliyetoka usingizini, maana wote walisinzia, kwa sababu usingizi mzito kutoka kwa BWANA uliwaangukia.
13 Kisha Daudi akaenda upande mwingine na akasimama juu ya mlima mbali sana; ukiwepo umbali mkubwa katikati yao.
14 Daudi akawapigia kelele watu hao na Abneri mwana Neri; akisema, “Hujibu neno, Abneri?” Ndipo Abneri akajibu na kusema, “Wewe ni nani unayempigia mfalme kelele?”
15 Daudi akamwambia Abneri, “Wewe siye mtu jasiri? Ni nani yuko kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukukaa macho kumlinda bwana wako mfalme? Kwa maana mtu fulani aliingia kumuua mfalme, bwana wako.
16 Jambo hili ulilolifanya siyo zuri. Kama BWANA aishivyo, unapaswa kufa kwa sababu hukumlinda bwana wako, mtiwa mafuta wa BWANA. Na sasa tazama ulipo mkuki wa mfalme, na jagi la maji lililokuwa kichwani pake.”
17 Sauli aliitambua sauti ya Daudi akasema, “Hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Daudi akasema, “Ni sauti yangu, mfalme, bwana wangu.”
18 Daudi akasema, “Kwa nini bwana wangu anamwandama mtumishi wake? Nimefanya nini? Mkononi mwangu kuna uovu gani?
19 Kwa hiyo sasa, nakusihi, bwana wangu mfalme asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama ni BWANA ndiye amekuchochea dhidi yangu, na aikubali sadaka; lakini kama ni wanadamu, na walaaniwe mbele za BWANA, maana leo wamenifukuza, nisishikamane na urithi wa BWANA; wameniambia, 'Nenda ukaabudu miungu mingine.'
20 Kwa hiyo, sasa, usiiachilie damu yangu ianguke ardhini mbali na uwepo wa BWANA; kwa kuwa mfalme wa Israeli ametoka nje kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware milimani.”
21 Kisha Sauli akasema, “Nimefanya dhambi. Rudi, Mwanangu, Daudi; maana sitakudhuru tena, kwa sababu leo maisha yangu yalikuwa yenye thamani machoni pako. Tazama, nimetenda upumbavu na nimekosa sana.”
22 Daudi akajibu na akasema, “Tazama, mkuki wako uko hapa, mfalme! Mruhusu kijana mmojawapo aje auchukue na aulete kwako.
23 Na BWANA amlipe kila mtu kwa ajili ya uadilifu wake na kwa uaminifu wake; kwa sababu leo BWANA alikuweka mkononi mwangu, lakini nisinge mpiga mtiwa mafuta wake.
24 Na tazama, kama maisha yako leo yalivyokuwa ya thamani machoni pangu, vivyo hivyo maisha yangu yathaminiwe sana machoni pa BWANA, na aweze kuniokoa katika shida zote.”
25 Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Na ubarikiwe, mwanangu Daudi, ili uweze kutenda mambo makuu, na hakika uweze kufanikiwa.” Ndipo Daudi akaenda zake, na Sauli akarudi kwake.