27
1 Daudi alisema moyoni mwake, “Basi, siku moja nitaangamia kwa mkono wa Sauli; hakuna jambo zuri kwangu kuliko kutoroka hadi nchi ya Wafilisti; Sauli atakata tamaa asinitafute tena ndani ya mipaka yote ya Israeli; kwa njia hii nitaponyoka kutoka mkono wake.”
2 Daudi akaondoka na kuvuka, akiwa pamoja na watu mia sita hadi kwa Akishi mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi.
3 Daudi akaishi na Akishi huko Gathi pamoja na watu wake, na kila mtu na familia yake, na Daudi akiwa na wake zake wawili, Ahinoamu Myezreeli, na Abigaili Mkarmeli aliyekuwa mke wa Nabali.
4 Sauli akaambiwa kuwa Daudi amekimbilia Gathi, hivyo hakumtafuta tena.
5 Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, wanipatie mahali katika mojawapo ya miji ya nchi, ili nikae huko: kwa nini mtumishi wako akae pamoja na wewe katika mji wa kifalme?”
6 Hivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi Ziklagi; ndiyo sababu mji wa Ziklagi ni mali ya wafalme wa Yuda hadi leo.
7 Idadi ya siku ambazo Daudi aliishi katika nchi ya Wafilisti ulikuwa mwaka mmoja na miezi minne.
8 Daudi na watu wake walizipiga sehemu mbalimbali, wakiteka nyara Wageshuri, Wagirizi, na Waamaleki; kwa maana mataifa hayo ndio walikuwa wakaaji wa nchi, kwa uelekeo wa kwenda Shuri hadi kufika nchi ya Misri. Walikuwa wamekaa katika nchi hiyo toka nyakati za zamani.
9 Daudi aliipiga nchi na hakumwacha mwanaume wala mwanamke akiwa hai; akatwaa kondoo, ng'ombe, punda, ngamia, na nguo; kisha alirudi na kufika tena kwa Akishi.
10 Ndipo Akishi humuuliza, “Je, leo umefanya mashambulizi dhidi ya nani?” Daudi humjibu, “Nimefanya dhidi ya kusini mwa Yuda,” au dhidi ya kusini mwa Wayerameeli,” au “dhidi ya kusini mwa Wakeni.”
11 Daudi asingemwacha mwanaume wala mwanamke akiwa hai awalete hadi Gathi, akisema, “ili wasije kututeta, 'Daudi amefanya hivi na vile.”' Hivi ndivyo alivyofanya kwa kipindi chote alichokaa katika nchi ya Wafilisti.
12 Akishi alimwamini Daudi, akisema, “Amesababisha watu wake Israeli wamchukie kabisa; kwa hiyo atakuwa mtumishi wangu milele.”