22
1 Daudi akamwimbia Yahwe maneno ya wimbo huu siku ile Yahwe alipomwokoa katika mkono wa adui zake wote na katika mkono wa Sauli.
2 Akaomba hivi, “Yahwe ni mwamba wangu, ngome yangu, aliyeniokoa.
3 Mungu ni mwamba wangu. Yeye ni kimbilio langu. Ngao yangu, pembe ya wokovu wangu, ngome yangu na kimbilio langu, aniokoaye na mabaya yote.
4 Nitamwita Yahwe, astahiliye kutukuzwa, nami nitaokolewa kutoka kwa adui zangu.
5 Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, mafuriko ya maji ya uharibifu yakanishinda.
6 Vifungo vya kuzimu vilinizunguka; kamba za mauti zikaninasa.
7 Katika shida yangu nalimwita Yahwe; nilimwita Mungu wangu; akaisikia sauti yangu katika hekalu lake, na kilio changu cha msaada kikafika masikioni mwake.
8 Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka. Misingi ya mbingu ikatetemeka na kutikiswa, kwa kuwa Mungu alikasirika.
9 Moshi ukatoka katika pua yake, na miale ya moto ikatoka katika kinywa chake. Makaa yakawashwa nayo.
10 Alizifungua mbingu akashuka, na giza totoro lilikuwa chini ya miguu yake.
11 Alipanda juu ya kerubi na kuruka. Alionekana katika mawingu ya upepo.
12 Naye akalifanya giza kuwa hema kumzunguka, akakusanya mawingu makubwa ya mvua angani.
13 Makaa ya moto yalidondoka mbele zake kutoka katika radi.
14 Yahwe alishuka kutoka katika mbingu. Aliyejuu alipiga kelele.
15 Alipiga mishale na kuwatawanya adui zake—miale ya radi na kuwasambaratisha.
16 Kisha njia za maji zikaonekana; misingi ya dunia ikawa wazi katika kilio cha vita ya Yahweh, katika sauti za pumzi ya pua zake.
17 Kutoka juu alifika chini; akanishikilia! Aliniondoa katika vilindi vya maji.
18 Aliniokoa kutoka kwa adui zangu wenye nguvu, kwao walionichukia, kwa maana walikuwa na nguvu sana kwangu.
19 Walikuja kinyume changu siku ya shida yangu, lakini Yahwe alikuwa msaada wangu.
20 Pia aliniweka mahali panapo nafasi. Aliniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
21 Yahwe amenituza kwa kipimo cha haki yangu; amenirejesha kwa kiwango cha usafi wa mikono yangu.
22 Kwa maana nimezishika njia za Yahwe na sijafanya uovu kwa kugeuka kutoka kwa Mungu.
23 Kwa kuwa maagizo yake yote ya haki yamekuwa mbele yangu; kwa kuwa sheria zake, sikujiepusha nazo.
24 Nimekuwa bila hatia mbele zake pia, na nimejiepusha na dhambi.
25 Kwa hiyo Yahwe amenirejesha kwa kiasi cha uadilifu wangu, kwa kipimo cha usafi wangu mbele zake.
26 Kwa mwaminifu, unajionesha kuwa mwaminifu; kwake asiye na hatia; unajionesha kuwa hauna hatia.
27 Kwa usafi unajionesha kuwa msafi, lakini kwa wakaidi unajionesha kuwa mkaidi.
28 Unaokoa walioteswa, lakini macho yako ni kinyume cha wenye kiburi, unawashusha chini.
29 Kwa maana wewe ni taa yangu, Yahwe. Yahwe huangaza katika giza langu.
30 Maana kwa ajili yake ninaweza kupita vipingamizi; kwa msaada wa Mungu wangu naweza kuruka juu ya ukuta.
31 Maana njia za Mungu ni kamilifu. Neno la Yahwe ni safi. Yeye ni ngao yao wanaomkimbilia.
32 Maana ni nani aliye Mungu isipokuwa Yahwe? Na ni nani aliyemwamba isipokuwa Mungu?
33 Mungu ni kimbilio langu, na umwongoza katika njia yake mtu asiye na hatia.
34 Huifanya myepesi miguu yangu kama kurungu na kuniweka katika vilima virefu.
35 Huifundisha mikono yangu kwa vita, na viganja vyangu kupinda upinde wa shaba.
36 Umenipa ngao ya wokovu wako, na matakwa yako yamenifanya mkuu.
37 Umeitengenezea miguu yangu nafasi chini yangu, hivyo miguu yangu haikujikwaa.
38 Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza. Sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
39 Niliwararua na kuwasambaratisha; hawawezi kuinuka. Wameanguka chini ya miguu yangu.
40 Unaweka nguvu ndani yangu kama mkanda kwa vita; unawaweka chini yangu wanaoinuka kinyume changu.
41 Ulinipa migongo ya shingo za adui zangu; niliwaangamiza kabisa wale wanaonichukia.
42 Walilia kwa msaada, lakini hakuna aliyewaokoa; walimlilia Yahwe, lakini hakuwajibu.
43 Niliwaponda katika vipande kama mavumbi juu ya ardhi, niliwakanyaga kama matope mitaani.
44 Umeniokoa pia kutoka katika mashutumu ya watu wangu. Umeniweka kama kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua wananitumikia.
45 Wageni walishurutishwa kuniinamia. Mara waliposikia kuhusu mimi, walinitii.
46 Wageni walikuja wakitetemeka kutoka katika ngome zao.
47 Yahwe anaishi! Mwamba wangu atukuzwe. Mungu na ainuliwe, mwamba wa wokovu wangu.
48 Huyu ndiye Mungu anilipiaye kisasi, awawekaye watu chini yangu.
49 Uniweka huru mbali na adui zangu. Hakika, uliniinua juu yao walioinuka kinyume changu. Uliniokoa kutoka kwa watu wenye ghasia.
50 Kwa hiyo nitakushukuru, Yahwe, kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.
51 Mungu hutoa ushindi mkuu kwa mfalme wake, na uonesha uaminifu wake wa kiagano kwa mtiwa mafuta wake, kwa Daudi na uzao wake daima.”