10
1 Mwombeni Yahwe mvua nyakati za kipupwe - Yahwe afanyaye mvua ya radi - naye hufanya mvua inyeshe kwa kila mmoja na uoto kondeni.
2 Kwani sanamu za wenye nyumba husema uongo; waganga hunena uongo; wanasema ndoto za udanganyifu na hutoa faraja tupu, hivyo wapotea kama kondoo na wanaumia kwa sababu hakuna mchungaji.
3 Gadhabu yangu inawaka dhidi ya wachungaji; ni mabeberu - viongozi - nitakao waadhibu. Yahwe wa majeshi atalihudumia pia kundi la kondoo wake, nyumba ya Yuda, na kuwafanya kama farasi wake wa vita!
4 Kutoka kwao litatoka jiwe kuu la pembeni; kutoka kwao kitatoka kigingi cha hema; kutoka kwao utatoka upinde wa vita; kutoka kwao watakuja viongozi wote kwa pamoja.
5 Watakuwa kama mashujaa wawakanyagao adui zao katika matope ya mitaani vitani; watafanya vita, kwa maana Yahwe yu pamoja nao, nao watawaabisha wapanda farasi wa vita.
6 Nitaitia nguvu nyumba ya Yuda na kuiokoa nyumba ya Yusufu; kwani nitawarejesha na kuwahurumia. Watakuwa kama nilikuwa sijawaondoa, kwani mimi ni Yahwe Mungu wao, nami nitawaitikia.
7 Ndipo Efraimu atakapokuwa kama shujaa, na mioyo yao itafurahi kama kwa mvinyo; wana wao wataona na kufurahi. Mioyo yao itanifurahia!
8 Nitawanong'oneza na kuwakusanya, kwani nitawaokoa, nao watakuwa wakuu kama walivyokuwa mwanzo!
9 Niliwapanda kati ya watu, lakini watanikumbuka katika nchi ya mbali, hivyo wao na wana wao wataishi na kurejea.
10 Kwa maana nitawarejesha kutoka nchi ya Misri na kuwakusanya kutoka Ashuru. Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni mpaka kutakapokuwa hakuna nafasi tena kwa ajili yao.
11 Nitapita katika bahari ya mateso yao; nitayapiga mawimbi ya bahari hiyo na nitavikausha vilindi vyote vya Nile. Utukufu wa Ashuru utashushwa chini, na fimbo ya Misri itakwenda mbali kutoka kwa Wamisri.
12 Nitawatia nguvu katika mimi mwenyewe, nao watatembea katika jina langu - asema Yahwe.