11
1 Fungua milango yako, ee Lebanoni, ili moto uteketeze mielezi yako!
2 Omboleza, enyi miti ya misonobari, kwani mierezi imeanguka! Kilichokuwa cha fahari kimeteketezwa! Ombolezeni, enyi mialoni ya Bashani, kwani msitu wenye nguvu umeshushwa.
3 Wachungaji wanapiga yowe, kwa kuwa utukufu wao umeharibiwa! Sauti ya mungurumo wa wana simba, kwa kuwa kiburi cha Mto Yordani kimeharibiwa!
4 Hivi ndivyo asemavyo Yahwe Mungu wangu, “Lichungeni kundi la kondoo lililotiyari kuchinjwa!
5 (Wanaowanunua wanawachinja bila kuhadhibiwa, nao wawauzao husema, 'Atukuzwe Yahwe! Nimetajirika! Kwa maana wachungaji wafanyao kazi kwa wenye kondoo hawawahurumii.)
6 Kwa maana hiyo sitawahurumia tena wenyeji wa nchi! - hivi ndivyo asemavyo Yahwe. Tazama! Mimi mwenyewe nipo tiyari kumwelekeza kila mtu katika mkono wa jirani yake na katika mkono wa mfalme wake, nao wataiharibu nchi na hakuna hata mmoja wao nitakayemwokoa kutoka katika mkono wao.”
7 Hivyo nikawa mchungaji wa kondoo walioamriwa kuchinjwa, kwa wanaowashughulikia kondoo. Nilichukua fimbo mbili; fimbo moja nikaiita “Neema” na nyingine nikaiita “Umoja.” Kwa njia hii niliwachunga kondoo.
8 Ndani ya mwezi mmoja niliwaangamiza wachungaji watatu, kwa maana sikuwavumilia tena, wao pia walinichukia.
9 Ndipo nilipowaambia wamiliki, “Sitafanya kazi kama mchungaji wenu tena. Wakondoo wafao - na wafe; kondoo wanaoangamizwa - na waangamizwe. Na kondoo wasaliao kila mmoja ale nyama ya jirani yake.”
10 Hivyo nikaichukua fimbo yangu “Neema” na nikaivunja kuvunja agano nililokuwa nimelifanya na kabila zangu zote.
11 Katika siku hiyo agano lilivunjwa, na wale wanaoshughulika na kondoo na waliokuwa wakiniangalia walifahamu kwamba Yahwe amesema.
12 Nikawaambia, “Ikiwa itawapendeza, nilipeni ujira wangu. Kama sivyo, msifanye hivyo.” Hivyo wakapima ujira wangu - vipande thelathini vya fedha.
13 Kisha Yahwe akaniambia, “Weka fedha katika hazina, thamani nzuri zaidi ambayo walikupa!” Hivyo nikachukua vipande thelathini vya fedha na kuviweka katika hazina ndani ya nyumbani Yahwe.
14 Kisha nikavunja fimbo yangu ya pili, “Umoja,” kuvunja undugu kati ya Yuda na Israeli.
15 Yahwe akaniambia, “Tena, chukua chombo cha mchungaji mpumbavu kwa ajili yako mwenyewe,
16 kwa maana tazama, niko tiyari kumweka mahali mchungaji katika nchi. Hataangalia kondoo wanaoangamia. Hatatafuta kondoo wapoteao, wala kuwaponya kondoo wachechemeao. Hatawalisha kondoo wenye afya, lakini atakula nyama ya kondoo walionona naye atapasua kwato zao.
17 Ole kwa wachungaji wasiofaa wanaoliacha kundi la kondoo! Upanga na uje dhidi ya mkono wake na jicho lake la kulia! Mkono wake na ukauke na jicho lake la kulia lipofuke!