14
1 Tazama! Siku ya Yahwe inakuja wakati mateka wenu watakapogawanywa katikati yenu.
2 Kwa maana nitayakusanya mataifa yote kinyume cha Yerusalemu kwa vita na mji utatekwa. Nyumba zitatekwa na wanawake watabakwa. Nusu ya mji itapelekwa matekani, lakini kumbukumbu ya watu haitaondolewa mjini.
3 Lakini Yahwe ataondoka na kufanya vita dhidi ya mataifa kama apigavyo vita katika siku ya vita.
4 Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, uliopo kando ya Yerusalemu upande wa mashariki. Mlima wa Mizeituni utagawanyika katikati kati ya mashariki na magharibi kwa bonde kubwa sana na nusu ya mlima itarudi nyuma kuelekea kaskazini na nusu kuelekea kusini.
5 Ndipo mtakapokimbia katika bonde kati ya milima ya Yahwe, kwa kuwa bonde kati ya hiyo milima litafika hata Azali. Mtakimbia kama siku mliyokimbia tetemeko la nchi siku za Uzia, mfalme wa Yuda. Ndipo Yahwe Mungu wangu atakapokuja na watakatifu wake wote.
6 Hakutakuwa na nuru katika siku hiyo, lakini hakuna baridi wala barafu.
7 Siku hiyo, siku aijuaye Yahwe peke yake, hakutakuwa tena na mchana wala usiku, kwani jioni itakuwa wakati wa nuru.
8 Siku hiyo maji yaliyo hai yatatiririka kutoka Yerusalemu. Nusu yake yatatiririka kuelekea bahari ya mashariki na nusu bahari ya magharibi, wakati wa masika na wakati wa kiangazi.
9 Yahwe atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Katika siku hiyo kutakuwa na Yahwe, Mungu mmoja, na jina lake pekee.
10 Nchi yote itakuwa kama Araba, kuanzia Geba hadi Rimoni kusini mwa Yerusalemu. Na Yerusalemu itaendelea kuwa juu. Ataishi mahali pake mwenyewe, kutoka lango la Benjamini hata mahali lilipokuwa lango la kwanza, hata Lango la Pembeni, na kutoka Mnara wa Hananeli hata shinikizo la mfalme.
11 Watu watakaa Yerusalemu na hakutakuwa na maangamizi kamili tena kutoka kwa Mungu dhidi yao. Yerusalemu itakuwa salama.
12 Hii itakuwa tauni ambayo kwayo Yahwe atawapiga jamaa zote za watu wapigao vita juu ya Yerusalemu: miili yao itaoza hata wakiwa wamesimama kwa miguu yao. Macho yao yataoza katika matundu yake na ndimi zao zitaoza katika vinywa vyao.
13 Siku hiyo ile hofu kuu kutoka kwa Yahwe itakuwa miongoni mwao. Kila mmoja ataushika mkono wa mwingine, na mkono wa mwingine utainuliwa kinyume cha mkono wa mwenzake.
14 Yuda pia atapigana na Yerusalemu. Watakusanya utajiri wa mataifa yote yanayowazunguka - dhahabu, fedha, na wingi wa nguo safi.
15 Tauni itakuwa pia juu ya farasi na nyumbu, ngamia na punda, na kila mnyama katika kambi hizo atapigwa kwa hilo pigo.
16 Kisha itakuwa wote watakaosalia katika mataifa yaliyo kinyume na Yerusalemu watakwenda mwaka kwa mwaka kumwabudu mfalme, Yahwe wa majeshi, na kutunza Sikukuu ya Vibanda.
17 Na itakuwa kwamba ikiwa mtu yeyote kutoka katika mataifa yote ya dunia haendi Yerusalemu kumwabudu mfalme, Yahwe wa majeshi, ndipo Yahwe hataleta mvua juu yao.
18 Na ikiwa nchi ya Misri hawatakwenda, ndipo hawatapata mvua. Tauni kutoka kwa Yahwe itayashambulia mataifa yote yasiyokwea kutunza Sikukuu ya Vibanda.
19 Hii itakuwa ni adhabu kwa Misri na adhabu kwa kila taifa lisilopanda kutunza Sikukuu ya Vibanda.
20 Lakini katika siku hiyo, kengele za farasi zitasema, “Jitengeni kwa ajili ya Yahwe,” na makalai katika nyumba ya Yahwe yatakuwa kama mabakuri mbele ya madhabahu.
21 Kwa kuwa kila chungu katika Yerusalemu na Yuda kitatengwa kwa ajili ya Yahwe wa majeshi na kila mmoja aletaye sadaka atakula ndani yake na kuyachemshia. Hakutakuwa na wafanyabiashara tena katika nyumba ya Yahwe wa majeshi siku hiyo.