13
Kurudishwa Kwa Sanduku La Mungu
(2 Samweli 6:1-11)
Daudi alishauriana na kila afisa wake, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia. Ndipo Daudi akaliambia kusanyiko lote la Israeli, “Kama mkiona ni vyema, na kama ni mapenzi ya Bwana Mungu wetu, tupeleke ujumbe kwa ndugu zetu wengine walio mbali na walio karibu katika nchi yote ya Israeli, pia kwa makuhani na Walawi walio pamoja nao katika miji yao na katika sehemu zao za malisho yao, waje waungane na sisi. Sisi na tulirudishe Sanduku la Mungu wetu kwetu kwa maana hatukujali wakati wa utawala wa Sauli.” Kusanyiko lote likakubaliana kufanya hivyo, kwa sababu ilionekana vyema kwa watu wote.
Basi Daudi akawakusanya Waisraeli wote, kuanzia Mto Shihori ulioko Misri hadi Lebo-Hamathi, ili kulileta Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu. Daudi akiwa pamoja na Waisraeli wote wakaenda Baala ya Yuda (yaani Kiriath-Yearimu) kulipandisha Sanduku la Mungu Bwana, yeye anayeketi katika kiti cha enzi kati ya makerubi: Sanduku linaloitwa kwa Jina lake, kutoka huko.
Wakalisafirisha Sanduku la Mungu kwa gari jipya la kukokotwa na maksai kutoka nyumba ya Abinadabu, Uza na Ahio wakiliongoza gari hilo. Daudi pamoja na Waisraeli wote walikuwa wanasifu kwa nguvu zao zote mbele za Mungu, kwa nyimbo na kwa vinubi, zeze, matari, matoazi na tarumbeta.
Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza akaunyoosha mkono wake ili kulizuia Sanduku, kwa sababu maksai walijikwaa. 10 Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Uza, akampiga kwa sababu aliuweka mkono wake kwenye Sanduku. Kwa hiyo akafa pale mbele za Mungu.
11 Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya Bwana ilifurika dhidi ya Uza, mahali pale pakaitwa Peres-Uza*Maana yake ni Gadhabu dhidi ya Uza. hadi leo.
12 Siku ile Daudi akamwogopa Mungu naye akauliza. “Nitawezaje kulichukua Sanduku la Mungu kwangu?” 13 Hakulichukua hilo Sanduku akae nalo katika Mji wa Daudi. Badala yake, akalipeleka nyumbani kwa Obed-Edomu, Mgiti. 14 Sanduku la Mungu likabaki pamoja na jamaa ya Obed-Edomu, nyumbani kwake kwa miezi mitatu, naye Bwana akaibariki nyumba yake pamoja na kila kitu alichokuwa nacho.

*13:11 Maana yake ni Gadhabu dhidi ya Uza.