25
Kuanguka Kwa Yerusalemu
(2 Nyakati 36:13-21; Yeremia 52:3-30)
1 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli, akiwa na jeshi lake lote, alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote. 2 Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia. 3 Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu. 4 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa, na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba. 5 Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia mfalme na kumpata katika sehemu tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika, 6 naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, mahali ambapo hukumu yake ilitangazwa. 7 Wakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Kisha wakayangʼoa macho yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
8 Mnamo siku ya saba ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme, afisa wa mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu. 9 Alichoma moto Hekalu la Bwana, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu. 10 Jeshi lote la Wakaldayo, chini ya jemadari wa askari walinzi wa mfalme, walivunja kuta zilizoizunguka Yerusalemu. 11 Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi akawapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli. 12 Lakini yule jemadari wa askari walinzi akawaacha baadhi ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
13 Wakaldayo walivunja vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Bwana. Hivyo wakaichukua hiyo shaba na kuipeleka Babeli. 14 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu. 15 Jemadari wa askari walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.
16 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Solomoni alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Bwana, ilikuwa na uzito usioweza kupimika. 17 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane.*Dhiraa 18 ni sawa na mita 8.2. Sehemu ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tatu†Dhiraa 3 ni sawa na mita 1.35. na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo ya kwanza.
18 Yule jemadari wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu. 19 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri watano wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji. 20 Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. 21 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe.
Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao.
22 Nebukadneza mfalme wa Babeli akamteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, awe msimamizi wa watu aliowaacha Yuda. 23 Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia kuwa mtawala, wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao. 24 Gedalia akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema, “Msiwaogope maafisa wa Kikaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu.”
25 Hata hivyo, katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania mwana wa Elishama, aliyekuwa wa uzao wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi, nao wakamuua Gedalia, na pia watu wa Yuda, pamoja na Wakaldayo waliokuwa naye huko Mispa. 26 Baada ya haya, watu wote kuanzia aliye mdogo sana hadi aliye mkubwa kabisa, pamoja na maafisa wa jeshi, wakakimbilia Misri kwa kuwaogopa Wakaldayo.
Yehoyakini Anaachiwa
(Yeremia 52:31-34)
27 Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, katika mwaka ule ambao Evil-Merodaki‡Pia aliitwa Ameli-Mariduki. alifanyika mfalme wa Babeli, alimwacha huru Yehoyakini kutoka gerezani siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili. 28 Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima zaidi kuliko wale wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli. 29 Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya mfungwa, na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula mezani mwa mfalme. 30 Siku kwa siku mfalme alimpa Yehoyakini posho siku zote za maisha yake.