49
Yakobo Abariki Wanawe
Ndipo Yakobo akawaita wanawe na kusema: “Kusanyikeni kunizunguka ili niweze kuwaambia lile litakalowatokea siku zijazo.
“Kusanyikeni na msikilize, enyi wana wa Yakobo,
msikilizeni baba yenu Israeli.
 
“Reubeni, wewe ni mzaliwa wangu wa kwanza,
nguvu zangu, tunda la kwanza la nguvu zangu,
umepita kwa heshima, umepita kwa uwezo.
Usiyezuiwa kama maji, basi hutakuwa mkuu tena,
kwa kuwa ulipanda kwenye kitanda cha baba yako,
kwenye kitanda changu na kukinajisi.
 
“Simeoni na Lawi ni wana ndugu:
panga zao ni silaha za jeuri.
Mimi na nisiingie katika baraza lao,
nami nisiunganike katika kusanyiko lao,
kwa kuwa wamewaua watu katika hasira yao,
walikata mishipa ya miguu ya mafahali
kama walivyopenda.
Hasira yao na ilaaniwe, kwa kuwa ni kali mno,
nayo ghadhabu yao ni ya ukatili!
Nitawatawanya katika Yakobo
Na kuwasambaza katika Israeli.
 
“Yuda, ndugu zako watakusifu;
mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako;
wana wa baba yako watakusujudia.
Ee Yuda, wewe ni mwana simba;
unarudi toka mawindoni, mwanangu.
Kama simba hunyemelea na kulala chini,
kama simba jike: nani athubutuye kumwamsha?
10 Fimbo ya ufalme haitaondoka kwa Yuda,
wala fimbo ya mtawala kati ya miguu yake,
hadi aje yeye ambaye milki ni yake,
ambaye utii wa mataifa ni wake.
11 Atamfunga punda wake katika mzabibu,
naye mwana-punda wake kwenye tawi lililo bora zaidi;
atafua mavazi yake katika divai,
majoho yake katika damu ya mizabibu.
12 Macho yake yatakuwa mekundu kwa divai,
meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa.
 
13 “Zabuloni ataishi pwani ya bahari
na kuwa bandari za kuegesha meli;
mpaka wake utapanuka kuelekea Sidoni.
 
14 “Isakari ni punda mwenye nguvu
ambaye amelala kati ya mizigo yake.
15 Aonapo palivyo pazuri mahali pake pa kupumzika
na jinsi nchi yake inavyopendeza,
atainamisha bega lake kwenye mzigo
na kujitolea kwa ajili ya kazi ngumu.
 
16 “Dani atahukumu watu wake kwa haki
kama mmoja wa makabila ya Israeli.
17 Dani atakuwa nyoka kando ya barabara,
nyoka mwenye sumu kando ya njia,
yule aumaye visigino vya farasi
ili yule ampandaye aanguke chali.
 
18 “Ee Bwana, nautafuta wokovu wako.
 
19 “Gadi atashambuliwa ghafula na kundi la washambuliaji,
lakini yeye atawageukia na kuwashinda kabisa.
 
20 “Chakula cha Asheri kitakuwa kinono,
naye atatoa chakula kitamu kimfaacho mfalme.
 
21 “Naftali ni kulungu jike aliyeachiwa huru
azaaye watoto wazuri.
 
22 “Yosefu ni mzabibu uzaao,
mzabibu uzaao ulio kando ya chemchemi,
ambao matawi yake hutanda ukutani.
23 Kwa uchungu wapiga mshale walimshambulia,
wakampiga mshale kwa ukatili.
24 Lakini upinde wake ulibaki imara,
mikono yake ikatiwa nguvu,
na mkono wa Mwenye Nguvu wa Yakobo,
kwa sababu ya Mchungaji, Mwamba wa Israeli,
25 kwa sababu ya Mungu wa baba yako, anayekusaidia,
kwa sababu ya Mwenyezi,* Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania. yeye anayekubariki
kwa baraka za mbinguni juu,
baraka za kilindi kilichoko chini,
baraka za matitini na za tumbo la uzazi.
26 Baraka za baba yako ni kubwa
kuliko baraka za milima ya kale,
nyingi kuliko vilima vya kale.
Baraka hizo zote na zikae juu ya kichwa cha Yosefu,
juu ya paji la yule mkuu miongoni mwa ndugu zake.
 
27 “Benyamini ni mbwa mwitu mlafi mwenye njaa kuu;
asubuhi hurarua mawindo yake,
jioni hugawa nyara.”
28 Haya yote ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli, na hivi ndivyo baba yao alivyowaambia alipowabariki, akimpa kila mmoja baraka inayomfaa.
Kifo Cha Yakobo
29 Ndipo alipowapa maelekezo haya: “Mimi niko karibu kukusanywa kwa watu wangu. Mnizike pamoja na baba zangu kwenye pango katika shamba la Efroni, Mhiti, 30 pango lililoko katika shamba la Makpela, karibu na Mamre huko Kanaani, ambalo Abrahamu alinunua kwa ajili ya mahali pa kuzikia kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba. 31 Huko ndiko Abrahamu na Sara mkewe walikozikwa, huko akazikwa Isaki na Rebeka mkewe, na huko nilimzika Lea. 32 Shamba hilo na pango lililoko ndani yake lilinunuliwa kutoka kwa Wahiti.”
33 Baada ya Yakobo kumaliza kutoa maelekezo hayo kwa wanawe, akarudisha miguu yake kitandani, akapumua pumzi ya mwisho, na akakusanywa kwa watu wake.

*49:25 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.