50
Basi Yosefu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu. Ndipo Yosefu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa ili asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze, wakatumia siku arobaini, kwa maana ndio muda uliotakiwa wa kutia dawa ili asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini.
Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yosefu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni, ‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’ ”
Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.”
Hivyo Yosefu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake na watu mashuhuri wote wa Misri. Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani kwa Yosefu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni. Magari makubwa na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana.
10 Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu; Yosefu akapumzika huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake. 11 Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu.* Abel-Mizraimu maana yake Maombolezo ya Wamisri.
12 Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza: 13 Wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Abrahamu alilinunua kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia. 14 Baada ya Yosefu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wamekwenda naye kumzika baba yake.
Yosefu Awaondolea Ndugu Zake Mashaka
15 Ndugu zake Yosefu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yosefu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?” 16 Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya: 17 ‘Hili ndilo mtakalomwambia Yosefu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yosefu akalia.
18 Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.”
19 Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu? 20 Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi. 21 Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawahakikishia na kusema nao kwa wema.
Kifo Cha Yosefu
22 Yosefu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka 110, 23 naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yosefu walipozaliwa.
24 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Abrahamu, Isaki na Yakobo.” 25 Naye Yosefu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.”
26 Kwa hiyo Yosefu akafa akiwa na umri wa miaka 110. Baada ya kumtia dawa ili asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.

*50:11 Abel-Mizraimu maana yake Maombolezo ya Wamisri.