26
Shauri Baya La Kumuua Yesu
(Marko 14:1-2; Luka 22:1-2; Yohana 11:45-53)
Yesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake, “Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.”
Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa. Wakafanya shauri ili kumkamata Yesu kwa siri na kumuua. Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.”
Yesu Anapakwa Mafuta Huko Bethania
(Marko 14:3-9; Yohana 12:1-8)
Yesu alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma, naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa; akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula.
Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini? Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.”
10 Yesu, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana. 11 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. 12 Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu. 13 Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”
Yuda Akubali Kumsaliti Yesu
(Marko 14:10-11; Luka 22:3-6)
14 Kisha mmojawapo wa wale kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa viongozi wa makuhani 15 na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. 16 Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu.
Yesu Ala Pasaka Pamoja Na Wanafunzi
(Marko 14:12-21; Luka 22:7-23; Yohana 13:21-30)
17 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
18 Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” 19 Hivyo wanafunzi wakafanya kama vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.
20 Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. 21 Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”
22 Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”
23 Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti. 24 Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!”
25 Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Rabi?”
Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”
Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana
(Marko 14:22-26; Luka 22:14-20; 1 Wakorintho 11:23-25)
26 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”
27 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28 Hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”
30 Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.
Yesu Atabiri Petro Kumkana
(Marko 14:27-31; Luka 22:31-34; Yohana 13:36-38)
31 Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu, ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:
“ ‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’
32 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
33 Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”
34 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
35 Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.
Yesu Anaomba Gethsemane
(Marko 14:32-42; Luka 22:39-46)
36 Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.” 37 Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. 38 Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”
39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”
40 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41 Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”
42 Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”
43 Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. 44 Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.
45 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. 46 Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
Yesu Akamatwa
(Marko 14:43-50; Luka 22:47-53; Yohana 18:3-12)
47 Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” 49 Mara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu.
50 Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”
Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu. 51 Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
52 Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. 53 Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54 Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”
55 Wakati huo, Yesu akawaambia ule umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? 56 Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.
Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu
(Marko 14:53-65; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)
57 Wale waliokuwa wamemkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika. 58 Lakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.
59 Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. 60 Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.
Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo 61 na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”
62 Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 63 Lakini Yesu akakaa kimya.
Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo,*Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. Mwana wa Mungu.”
64 Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
65 Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru. 66 Uamuzi wenu ni gani?”
Wakajibu, “Anastahili kufa.”
67 Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi 68 na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”
Petro Amkana Bwana Yesu
(Marko 14:66-72; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)
69 Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mtumishi mmoja wa kike akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”
70 Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”
71 Alipotoka nje kufika kwenye lango, mtumishi mwingine wa kike alimwona, akawaambia watu waliokuwepo, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”
72 Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”
73 Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.”
74 Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!”
Papo hapo jogoo akawika. 75 Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.

*26:63 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.