27
Yesu Aletwa Mbele Ya Pilato
(Marko 15:1; Luka 23:1-2; Yohana 18:28-32)
Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumuua. Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala wa Kirumi.
Yuda Ajinyonga
(Matendo 1:18-19)
Yuda, ambaye alikuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”
Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”
Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.
Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. Ndipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli, 10 wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”
Yesu Mbele Ya Pilato
(Marko 15:2-15; Luka 23:3-25; Yohana 18:33–19:16)
11 Wakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.”
12 Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. 13 Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” 14 Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.
15 Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. 16 Wakati huo alikuwepo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. 17 Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?” 18 Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.
19 Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”
20 Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Yesu auawe.
21 Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”
Wakajibu, “Baraba.”
22 Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?”
Wakajibu wote, “Msulubishe!”
23 Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”
Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”
24 Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”
25 Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”
26 Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Askari Wamdhihaki Yesu
(Marko 15:16-20; Yohana 19:2-3)
27 Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitorio* Praitorio maana yake ni makao makuu ya mtawala, jumba la kifalme lililokuwa linakaliwa na Pontio Pilato huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu. na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka. 28 Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha 29 wakasokota taji ya miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 30 Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. 31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.
Yesu Asulubishwa
(Marko 15:21-32; Luka 23:26-43; Yohana 19:17-27)
32 Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. 33 Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). 34 Hapo wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa. 35 Walipokwisha kumsulubisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] 36 Kisha wakaketi, wakamchunga. 37 Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi. 38 Wanyangʼanyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. 39 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao 40 na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.”
41 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamdhihaki wakisema, 42 “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, nasi tutamwamini. 43 Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” 44 Hata wale wanyangʼanyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.
Kifo Cha Yesu
(Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; Yohana 19:28-30)
45 Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote. 46 Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
47 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.”
48 Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe. 49 Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.”
50 Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.
51 Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. 52 Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. 53 Wakatoka makaburini, na baada ya Yesu kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.
54 Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa, wakasema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
55 Walikuwako wanawake huko wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. 56 Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo na Yosefu, na mama yao wana wa Zebedayo.
Maziko Ya Yesu
(Marko 15:42-47; Luka 23:50-56; Yohana 19:38-42)
57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58 Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe. 59 Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, 60 na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake. 61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwepo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.
Walinzi Pale Kaburini
62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato 63 na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu wakati alikuwa bado hai alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ 64 Kwa hiyo uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti mpaka baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”
65 Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadri mwezavyo.” 66 Kwa hiyo wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.

*27:27 Praitorio maana yake ni makao makuu ya mtawala, jumba la kifalme lililokuwa linakaliwa na Pontio Pilato huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu.