Zaburi 83
Maombi Kwa Ajili Ya Kushindwa Kwa Adui Wa Israeli
Wimbo. Zaburi ya Asafu.
1 Ee Mungu, usinyamaze kimya,
usinyamaze, Ee Mungu, usitulie.
2 Tazama watesi wako wanafanya fujo,
jinsi adui zako wanavyoinua vichwa vyao.
3 Kwa hila, wanafanya shauri dhidi ya watu wako,
wanafanya shauri baya dhidi ya wale unaowapenda.
4 Wanasema, “Njooni, tuwaangamize kama taifa,
ili jina la Israeli lisikumbukwe tena.”
5 Kwa nia moja wanapanga mashauri mabaya pamoja,
wanafanya muungano dhidi yako,
6 mahema ya Edomu na Waishmaeli,
ya Wamoabu na Wahagari,
7 Gebali,*Yaani Bubilo, mji wa zamani sana wa Ufoinike (kama kilomita 80 kaskazini mwa Beiruti). Amoni na Amaleki,
Ufilisti, pamoja na watu wa Tiro.
8 Hata Ashuru wameungana nao
kuwapa nguvu wazao wa Loti.
9 Uwatendee kama vile ulivyowatendea Midiani,
na kama vile ulivyowatendea Sisera na Yabini
hapo kijito cha Kishoni,
10 ambao waliangamia huko Endori
na wakawa kama takataka juu ya nchi.
11 Wafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu,
watawala wao kama Zeba na Salmuna,
12 ambao walisema, “Na tumiliki nchi
ya malisho ya Mungu.”
13 Ee Mungu wangu, wapeperushe kama mavumbi ya kisulisuli,
kama makapi yapeperushwayo na upepo.
14 Kama vile moto uteketezavyo msitu
au mwali wa moto unavyounguza milima,
15 wafuatilie kwa tufani yako
na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.
16 Funika nyuso zao kwa aibu
ili watu walitafute jina lako, Ee Bwana.
17 Wao na waaibishwe na kufadhaishwa milele,
na waangamie kwa aibu.
18 Hebu wajue kwamba wewe, ambaye jina lako ni Bwana,
kwamba wewe peke yako ndiwe Uliye Juu Sana ya dunia yote.