Zaburi 84
Kuionea Shauku Nyumba Ya Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya wana wa Kora.
1 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
makao yako yapendeza kama nini!
2 Nafsi yangu inatamani sana,
naam, hata kuona shauku,
kwa ajili ya nyua za Bwana;
moyo wangu na mwili wangu
vinamlilia Mungu Aliye Hai.
3 Hata shomoro amejipatia makao,
mbayuwayu amejipatia kiota
mahali awezapo kuweka makinda yake:
mahali karibu na madhabahu yako,
Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
Mfalme wangu na Mungu wangu.
4 Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,
wanaokusifu wewe daima.
5 Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako,
na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao.
6 Wanapopita katika Bonde la Baka,*Yaani Bonde la Vilio.
hulifanya mahali pa chemchemi,
pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi.†Au: baraka.
7 Huendelea toka nguvu hadi nguvu,
hadi kila mmoja afikapo
mbele za Mungu huko Sayuni.
8 Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, sikia maombi yangu;
nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.
9 Ee Mungu, uitazame ngao yetu,
mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako.
10 Siku moja katika nyua zako ni bora
kuliko siku elfu mahali pengine;
afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu
kuliko kukaa katika mahema ya waovu.
11 Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao,
Bwana hutoa wema na heshima;
hakuna kitu chema anachowanyima
wale ambao hawana hatia.
12 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
heri ni mtu yule anayekutumaini wewe.