13
Kurudishwa kwa Sanduku la Mungu
(2 Samweli 6:1-11)
1 Daudi alishauriana na kila kiongozi wake, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia. 2 Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote la Israeli, “Mkiona ni vyema, na kama ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, tupeleke ujumbe kwa ndugu zetu wengine walio mbali na walio karibu katika nchi yote ya Israeli, pia kwa makuhani na Walawi walio pamoja nao katika miji yao na maeneo ya malisho ya miji hiyo, waje waungane na sisi. 3 Sisi na tulirudishe Sanduku la Mungu wetu kwetu kwa maana hatukujali wakati wa utawala wa Sauli.” 4 Kusanyiko lote wakakubaliana kufanya hivyo, kwa sababu ilionekana vyema kwa watu wote.
5 Basi Daudi akawakusanya Waisraeli wote, kuanzia Mto Shihori ulioko Misri hadi Lebo-Hamathi, ili kulileta Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu. 6 Daudi akiwa pamoja na Waisraeli wote wakaenda Baala ya Yuda (yaani Kiriath-Yearimu) kulipandisha Sanduku la Mungu Mwenyezi Mungu, yeye anayeketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi: Sanduku linaloitwa kwa Jina lake.
7 Wakalisafirisha Sanduku la Mungu kwa gari jipya la kukokotwa kutoka nyumba ya Abinadabu; nao Uza na Ahio waliliongoza gari hilo. 8 Daudi pamoja na Waisraeli wote walikuwa wanasifu kwa nguvu zao zote mbele za Mungu, kwa nyimbo na kwa vinubi, zeze, matari, matoazi na tarumbeta.
9 Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza akaunyoosha mkono wake ili kulizuia Sanduku, kwa sababu maksai walijikwaa. 10 Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Uza, akampiga kwa sababu aliuweka mkono wake kwenye Sanduku. Kwa hiyo akafa pale mbele za Mungu.
11 Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ilifurika dhidi ya Uza, mahali pale pakaitwa Peres-Uza*maana yake Gadhabu dhidi ya Uza hadi leo.
12 Siku ile Daudi akamwogopa Mungu naye akauliza. “Nitawezaje kulichukua Sanduku la Mungu kwangu?” 13 Hakulichukua hilo Sanduku akae nalo katika Mji wa Daudi. Badala yake, akalipeleka nyumbani mwa Obed-Edomu, Mgiti. 14 Sanduku la Mungu likakaa kwa jamaa ya Obed-Edomu, nyumbani mwake kwa miezi mitatu, naye Mwenyezi Mungu akaibariki nyumba yake pamoja na kila kitu alichokuwa nacho.