14
Nyumba ya Daudi na jamaa yake
(2 Samweli 5:11-16)
1 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, waashi na maseremala ili kumjengea jumba la kifalme. 2 Naye Daudi akatambua kwamba Mwenyezi Mungu amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na kwamba ufalme wake umetukuzwa kwa ajili ya Israeli, watu wake.
3 Huko Yerusalemu Daudi akaoa wake wengine zaidi na akawa baba wa wana wengi wa kiume na wa kike. 4 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani, 5 Ibihari, Elishua, Elpeleti, 6 Noga, Nefegi, Yafia, 7 Elishama, Beeliada na Elifeleti.
Daudi awashinda Wafilisti
(2 Samweli 5:17-25)
8 Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli yote, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akatoka ili kwenda kukabiliana nao. 9 Basi Wafilisti walikuwa wameingia na kushambulia Bonde la Warefai, 10 Hivyo Daudi akamuuliza Mungu: “Je, niende kuwashambulia hao Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”
Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.”
11 Hivyo Daudi pamoja na watu wake wakakwea hadi Baal-Perasimu, akawashinda huko. Akasema, “Kama maji yanavyofurika, Mungu amewafurikia adui zangu kwa kutumia mkono wangu.” Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Baal-Perasimu. 12 Wafilisti walikuwa wametupa miungu yao huko, naye Daudi akaamuru iteketezwe kwa moto.
13 Kwa mara nyingine Wafilisti wakavamia lile bonde; 14 hivyo Daudi akamuuliza Mungu tena, naye Mungu akamjibu, “Usiwafuate moja kwa moja, bali wazungukie na uwashambulie kutoka mbele ya hiyo miti ya miforosadi. 15 Mara utakaposikia sauti ya kutembea vileleni vya miti ya miforosadi, basi utoke upigane vita, kwa sababu hiyo itaonesha kwamba Mungu amekutangulia ili kupiga jeshi la Wafilisti.” 16 Kwa hiyo Daudi akafanya kama alivyoagizwa na Mungu, wakalipiga jeshi la Wafilisti kuanzia Gibeoni hadi Gezeri.
17 Hivyo umaarufu wa Daudi ukaenea katika kila nchi, naye Mwenyezi Mungu akayafanya mataifa yote kumwogopa Daudi.