22
1 Ndipo Daudi akasema, “Nyumba ya Bwana Mwenyezi Mungu itakuwa mahali hapa, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Israeli.”
Maandalizi kwa ajili ya Hekalu
2 Kwa hiyo Daudi akatoa amri wakusanyike wageni wote walioishi Israeli, na kutoka miongoni mwao, akaweka waashi ili kuchonga mawe kwa ajili ya kujenga nyumba ya Mungu. 3 Daudi akatoa chuma tele ili kutengenezea misumari kwa ajili ya mafungo ya malango ya nyumba na shaba tele isiyopimika. 4 Pia akatoa magogo ya mwerezi yasiyohesabika, kwa kuwa Wasidoni na Watiro walikuwa wamemletea Daudi idadi kubwa ya mierezi.
5 Daudi akasema, “Mwanangu Sulemani bado ni mdogo wa umri na hana uzoefu. Nyumba itakayojengwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu inatakiwa iwe yenye uzuri mwingi na sifa na fahari mbele ya mataifa yote. Kwa hiyo nitaifanyia matayarisho.” Daudi akafanya matayarisho makubwa kabla ya kifo chake.
6 Kisha akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza kujenga nyumba kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 7 Daudi akamwambia Sulemani: “Mwanangu, nilikuwa na jambo hili ndani ya moyo wangu, kujenga nyumba kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wangu. 8 Lakini neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema: ‘Wewe umemwaga damu nyingi na kupigana vita vingi. Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu. 9 Lakini utakuwa na mwana ambaye atakuwa mtu wa amani na utulivu, nami nitampa utulivu mbele ya adui zake wote pande zote. Jina lake ataitwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu wakati wa utawala wake. 10 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu. Yeye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. Nami nitakiimarisha kiti chake cha utawala juu ya Israeli milele.’
11 “Sasa, mwanangu, Mwenyezi Mungu awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kama alivyosema utafanya. 12 Mwenyezi Mungu na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika Torati ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. 13 Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Mwenyezi Mungu alizompa Musa kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.
14 “Nimejitaabisha sana ili kupata mahitaji kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu: talanta elfu mia moja*Talanta 100,000 ni sawa na tani 3,750. za dhahabu, talanta milioni moja†Talanta 1,000,000 ni sawa na tani 37,500. za fedha, na kiasi kisichopimika cha shaba na chuma, pia mbao na mawe. Nawe unaweza kuviongeza. 15 Unao wafanyakazi wengi: Wachonga mawe, waashi na maseremala, pamoja na watu walio na ustadi katika kila kazi 16 wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma, mafundi wasiohesabika. Sasa basi anza kazi hii, naye Mwenyezi Mungu awe pamoja nawe.”
17 Kisha Daudi akawaamuru viongozi wote wa Israeli wamsaidie Sulemani mwanawe. 18 Akawaambia, “Je, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, si yuko pamoja na ninyi? Pia si amewapa amani pande zote? Kwa maana amewatia wenyeji wa nchi mkononi mwangu, nayo nchi iko chini ya Mwenyezi Mungu na watu wake. 19 Sasa itoeni mioyo yenu na nafsi zenu katika kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Anzeni kujenga Maskani ya Bwana Mwenyezi Mungu, ili mweze kulileta Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na vyombo vitakatifu vya Mungu katika Hekalu litakalojengwa kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu.”