23
Jamaa za Walawi na utendaji wao
Daudi alipokuwa mzee aliyeshiba siku, akamfanya Sulemani mwanawe kuwa mfalme juu ya Israeli.
Pia akawakusanya viongozi wote wa Israeli, pamoja na makuhani na Walawi. Walawi waliokuwa na umri wa miaka thelathini au zaidi walihesabiwa, nayo hesabu ya wanaume ilikuwa elfu thelathini na nane. Daudi akasema, “Miongoni mwa hawa, elfu ishirini na nne watasimamia kazi ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na elfu sita watakuwa maafisa na waamuzi, na elfu nne watakuwa mabawabu, na wengine elfu nne watamsifu Mwenyezi Mungu kwa ala za uimbaji nilizotoa kwa ajili ya kusudi hilo.”
 
Daudi akawagawa Walawi katika makundi kufuatana na wana wa Lawi: Gershoni, Kohathi na Merari.
Wagershoni
Wana wa Wagershoni walikuwa wawili:
Ladani na Shimei.
Wana wa Ladani walikuwa watatu:
Yehieli wa kwanza, Zethamu na Yoeli.
Wana wa Shimei walikuwa watatu:
Shelomothi*au Shelomithi, Hazieli na Harani.
Hawa watatu walikuwa viongozi wa jamaa za Ladani.
10 Nao wana wa Shimei walikuwa:
Yahathi, Zinaau Ziza, Yeushi na Beria.
Hawa walikuwa wana wa Shimei: wanne kwa jumla.
11 Yahathi alikuwa wa kwanza na Ziza wa pili, lakini Yeushi na Beria hawakuwa na wana wengi; kwa hiyo walihesabiwa kama jamaa moja, wakapewa wajibu kwa pamoja.
Wakohathi
12 Wana wa Kohathi walikuwa:
Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli: wanne kwa jumla.
13 Wana wa Amramu walikuwa:
Haruni na Musa.
Haruni waliwekwa wakfu, yeye na wazao wake milele, wawe wakiweka wakfu vitu ambavyo ni vitakatifu mno, kutoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu, kuhudumu mbele zake na kubariki katika Jina la Mwenyezi Mungu milele. 14 Wana wa Musa mtu wa Mungu walihesabiwa kama sehemu ya kabila la Lawi.
15 Wana wa Musa walikuwa:
Gershomu na Eliezeri.
16 Wazao wa Gershomu:
Shebueli alikuwa wa kwanza.
17 Wazao wa Eliezeri:
Rehabia alikuwa wa kwanza.
Eliezeri alikuwa na mwana mmoja tu, lakini wana wa Rehabia walikuwa wengi sana.
18 Wana wa Ishari:
Shelomithi alikuwa wa kwanza.
19 Wana wa Hebroni walikuwa:
Yeria alikuwa wa kwanza, wa pili Amaria,
wa tatu Yahazieli, na wa nne Yekameamu.
20 Wana wa Uzieli walikuwa:
Mika wa kwanza na Ishia wa pili.
Wamerari
21 Wana wa Merari walikuwa:
Mahli na Mushi.
Wana wa Mahli walikuwa:
Eleazari na Kishi.
22 Eleazari akafa bila ya kuwa na wana: alikuwa na binti tu. Binamu zao, wana wa Kishi, wakawaoa.
23 Wana wa Mushi:
Mahli, Ederi na Yeremothi; wote walikuwa watatu.
 
24 Hawa walikuwa wazao wa Lawi kwa jamaa zao. Wakuu wa jamaa kama walivyoandikwa kwa majina yao na kuhesabiwa kila mmoja, yaani wenye uwezo wa kufanya kazi kuanzia miaka ishirini au zaidi, waliohudumu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. 25 Kwa maana Daudi alikuwa amesema, “Kwa vile Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, amewapa watu wake amani, na amekuja kuishi Yerusalemu milele, 26 Walawi hawahitaji tena kubeba Maskani wala chombo chochote cha utumishi wake.” 27 Kulingana na maagizo ya mwisho ya Daudi, Walawi walihesabiwa kuanzia umri wa miaka ishirini au zaidi.
 
28 Wajibu wa Walawi ulikuwa kuwasaidia wazao wa Haruni kuhudumu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu: Kuwa wasimamizi wa nyua, vyumba vya pembeni, kutakasa vyombo vitakatifu na utendaji mwingine wowote katika nyumba ya Mungu. 29 Walikuwa wasimamizi wa mikate iliyowekwa mezani, unga kwa ajili ya sadaka za nafaka, mikate myembamba isiyotiwa chachu, uokaji na uchanganyaji, pamoja na vipimo vyote vya wingi na ukubwa. 30 Pia ulikuwa wajibu wao kila asubuhi kumshukuru na kumsifu Mwenyezi Mungu. Iliwapasa pia kufanya hivyo jioni 31 na wakati wowote sadaka za kuteketezwa zilipotolewa kwa Mwenyezi Mungu siku za Sabato na kwenye sikukuu za Mwezi Mwandamo na katika sikukuu nyingine zilizoamriwa. Iliwapasa kuhudumu mbele za Mwenyezi Mungu mara kwa mara kwa idadi maalum na kwa namna waliyokuwa wamepewa maelekezo.
32 Hivyo Walawi wakafanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, katika Mahali Patakatifu chini ya uongozi wa ndugu zao wazao wa Haruni, kwa ajili ya utumishi katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.

*23:9 au Shelomithi

23:10 au Ziza