29
Matoleo kwa ajili ya ujenzi wa Hekalu
Ndipo Mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote: “Mwanangu Sulemani, yeye ambaye Mungu amemchagua, ni kijana mdogo na asiye na uzoefu. Kazi hii ni kubwa, kwa sababu Hekalu hili la fahari si kwa ajili ya mwanadamu bali ni kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu. Kwa uwezo wangu wote nimetenga mali kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu: dhahabu kwa kazi za dhahabu, fedha kwa ajili ya fedha, shaba kwa kazi za shaba, chuma kwa kazi za chuma na miti kwa kazi za miti, vivyo hivyo vito vya shohamu kwa ajili ya kutia kwenye vijalizo, almasi, mawe ya rangi mbalimbali, aina zote za vito vya thamani na marumaru; haya yote kwa wingi mno. Zaidi ya hayo, kwa kujitolea kwangu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, sasa ninatoa hazina zangu mwenyewe za dhahabu na fedha kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, zaidi ya mali niliyotoa kwa ajili ya Hekalu hili takatifu: talanta elfu tatu*Talanta 3,000 ni sawa na tani 110. za dhahabu (dhahabu ya Ofiri), na talanta elfu sabaTalanta 7,000 ni sawa na tani 260. za fedha safi iliyosafishwa, kwa ajili ya kufunika kuta za Hekalu, kwa kazi ya dhahabu na kazi ya fedha na kwa kazi yote itakayofanywa na mafundi. Basi, ni nani anayependa kujitoa kwa Mwenyezi Mungu leo?”
Ndipo viongozi wa jamaa, maafisa wa makabila ya Israeli, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, pamoja na maafisa waliokuwa wasimamizi wa kazi za mfalme wakatoa kwa hiari.
Wakatoa kwa ajili ya kazi ya Hekalu la Mungu talanta elfu tanoTalanta 5,000 ni sawa na tani 190. na darkoni elfu kumi§Darkoni 10,000 ni sawa na kilo 84. za dhahabu, talanta elfu kumi*Talanta 10,000 ni sawa na tani 375. za fedha, talanta elfu kumi na naneTalanta 18,000 ni sawa na tani 675. za shaba, na talanta elfu mia mojaTalanta 100,000 ni sawa na tani 3,750. za chuma. Kila mmoja aliyekuwa na vito vya thamani akavitoa katika hazina ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, chini ya uangalizi wa Yehieli Mgershoni. Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa Mwenyezi Mungu. Mfalme Daudi pia akafurahi sana.
Maombi ya Daudi
10 Daudi akamhimidi Mwenyezi Mungu mbele ya kusanyiko lote, akisema:
“Uhimidiwe wewe, Ee Mwenyezi Mungu,
Mungu wa Israeli baba yetu,
tangu milele hata milele.
11 Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Mwenyezi Mungu,
na utukufu na enzi na uzuri,
kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani
ni chako wewe.
Ee Mwenyezi Mungu, ufalme ni wako;
umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.
12 Utajiri na heshima vyatoka kwako;
wewe ndiwe unayetawala vitu vyote.
Mikononi mwako kuna nguvu na uweza
ili kuinua na kuwapa wote nguvu,
13 Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru
na kulisifu Jina lako tukufu.
14 “Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vinavyotoka mkononi mwako. 15 Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini. 16 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako. 17 Ninajua, Mungu wangu, kwamba wewe huujaribu moyo na unapendezwa na unyofu. Vitu hivi vyote nimetoa kwa hiari na kwa moyo mnyofu. Nami sasa nimeona kwa furaha jinsi watu wako walio hapa kwa hiari yao walivyokutolea wewe. 18 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu Ibrahimu, Isaka na Israeli, weka shauku hii ndani ya mioyo ya watu wako daima na uifanye mioyo yao iwe na uaminifu kwako. 19 Nawe umpe mwanangu Sulemani kujitolea kwako kwa moyo wote ili kuzishika amri zako, masharti yako, maagizo yako na kufanya kila kitu ili kujenga Hekalu hili la fahari ambalo kwa ajili yake nimetoa.”
20 Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, “Mhimidini Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.” Hivyo wote wakamhimidi Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao. Wakasujudu, na nyuso zao zikagusa chini mbele za Mwenyezi Mungu na mfalme.
Sulemani akubalika kuwa mfalme
21 Siku ya pili yake, wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu na sadaka za kuteketezwa: mafahali elfu moja, kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo dume elfu moja, pamoja na sadaka za vinywaji, na sadaka nyingine nyingi sana kwa ajili ya Israeli yote. 22 Wakala na kunywa kwa furaha kubwa mbele za Mwenyezi Mungu siku ile.
Wakamtawaza Sulemani mwana wa Daudi mara ya pili kuwa mfalme, wakampaka mafuta mbele za Mwenyezi Mungu ili awe mfalme na Sadoki kuwa kuhani. 23 Sulemani akaketi kwenye kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yake. Akafanikiwa sana, na Waisraeli wote wakamtii. 24 Maafisa wote na mashujaa, pamoja na wana wote wa Daudi, wakaahidi kumtii Mfalme Sulemani.
25 Mwenyezi Mungu akamtukuza sana Sulemani mbele ya Waisraeli wote na kumvika fahari ya kifalme ambayo hakuna mfalme yeyote wa Israeli kabla yake aliwahi kuwa nayo.
Muhtasari wa utawala wa Daudi
26 Daudi mwana wa Yese alikuwa mfalme wa Israeli yote. 27 Alitawala Israeli kwa miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na tatu.
28 Daudi akafa akiwa mzee mwenye umri mwema, akiwa ameshiba siku, utajiri na heshima. Naye Sulemani mwanawe akawa mfalme baada yake.
29 Kuhusu matukio ya utawala wa Mfalme Daudi, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kumbukumbu za mwonaji Samweli, na kumbukumbu za nabii Nathani na kumbukumbu za mwonaji Gadi, 30 pamoja na habari zote za utawala wake, nguvu zake na matukio yaliyompata yeye, na Israeli, na falme za nchi nyingine zote.

*29:4 Talanta 3,000 ni sawa na tani 110.

29:4 Talanta 7,000 ni sawa na tani 260.

29:7 Talanta 5,000 ni sawa na tani 190.

§29:7 Darkoni 10,000 ni sawa na kilo 84.

*29:7 Talanta 10,000 ni sawa na tani 375.

29:7 Talanta 18,000 ni sawa na tani 675.

29:7 Talanta 100,000 ni sawa na tani 3,750.