2 Mambo Ya Nyakati
1
Sulemani aomba hekima
(1 Wafalme 3:1-15)
1 Sulemani mwana wa Daudi alijiimarisha katika ufalme wake, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, naye akamfanya mkuu sana.
2 Ndipo Sulemani akasema na Waisraeli wote, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, waamuzi na viongozi wote katika Israeli, pamoja na wakuu wa jamaa. 3 Naye Sulemani na kusanyiko lote wakakwea hadi mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. Hema la Kukutania la Mungu, ambalo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alikuwa amelitengeneza huko jangwani, lilikuwa Gibeoni. 4 Basi Daudi alikuwa amelipandisha Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu hadi mahali alipokuwa amepatengeneza kwa ajili yake, kwa sababu alikuwa amesimamisha hema kwa ajili ya hilo Sanduku huko Yerusalemu. 5 Lakini yale madhabahu ya shaba ambayo Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, alikuwa ametengeneza yalikuwa huko Gibeoni mbele ya Maskani ya Mwenyezi Mungu, hivyo Sulemani na kusanyiko lote walimtafuta Mungu huko. 6 Sulemani akapanda huko yalikokuwa madhabahu ya shaba mbele za Mwenyezi Mungu katika Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu elfu moja za sadaka za kuteketezwa juu yake.
7 Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani na kumwambia, “Omba lolote utakalo nikupe.”
8 Sulemani akamjibu Mungu, “Umemwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, nawe umeniweka niwe mfalme mahali pake. 9 Sasa, Bwana Mwenyezi Mungu, ahadi yako kwa baba yangu Daudi na ithibitike, kwa kuwa umenifanya mimi mfalme juu ya watu ambao ni wengi kama mavumbi ya nchi. 10 Nakuomba unipe hekima na maarifa, ili niweze kuongoza watu hawa, kwa kuwa ni nani awezaye kutawala hawa watu wako walio wengi hivi?”
11 Mungu akamwambia Sulemani, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao, 12 kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.”
Fahari ya Sulemani
(1 Wafalme 10:26-29)
13 Ndipo Sulemani akaenda Yerusalemu kutoka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kutoka mbele ya Hema la Kukutania. Naye akatawala Israeli.
14 Sulemani akakusanya magari ya vita na farasi. Alikuwa na magari elfu moja mia nne, na farasi elfu kumi na mbili, ambayo aliyaweka katika miji ya magari, na mengine akawa nayo huko Yerusalemu. 15 Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa vitu vya kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima. 16 Farasi wa Sulemani waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue*yaani Kilikia. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue. 17 Waliagiza magari ya vita kutoka Misri kwa bei ya shekeli mia sita†Shekeli 600 ni sawa na kilo 7. za fedha, na farasi kwa shekeli mia moja na hamsini‡Shekeli 150 ni sawa na kilo 1.7.. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu.