2
Maandalizi ya ujenzi wa Hekalu
(1 Wafalme 5:1-18)
Sulemani akatoa amri kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe. Sulemani akaandika watu elfu sabini kuwa wachukuzi wa mizigo, na watu elfu themanini kuwa wachonga mawe vilimani, na watu elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao.
Sulemani akapeleka ujumbe huu kwa Mfalme Hiramu wa Tiro:
“Unitumie magogo ya mwerezi kama ulivyomfanyia baba yangu Daudi wakati ulipompelekea mierezi ya kujenga jumba lake la kifalme la kuishi. Sasa ninakaribia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, na kuliweka wakfu kwake kwa ajili ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri mbele zake, mahali pa kuweka mikate ya Wonesho kwa kufuata utaratibu na kwa ajili ya mahali pa kutolea sadaka za kuteketezwa kila siku asubuhi na jioni, siku za Sabato na Mwezi Mwandamo pia katika sikukuu zilizoamriwa za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Hili ni agizo la kudumu kwa ajili ya Waisraeli.
“Hekalu nitakalolijenga litakuwa kubwa, kwa sababu Mungu wetu ni mkuu kuliko miungu mingine yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea Hekalu, maadamu mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kumtosha? Mimi ni nani basi hata nimjengee Hekalu, isipokuwa liwe tu mahali pa kutolea dhabihu za kuteketezwa mbele zake?
“Hivyo basi nitumie mtu mwenye ustadi wa kufanya kazi ya kutengeneza dhahabu na fedha, shaba na chuma, nyuzi za rangi ya zambarau, nyekundu na buluu, mwenye uzoefu wa kutia nakshi, ili afanye kazi Yuda na Yerusalemu pamoja na mafundi wangu wenye ustadi, ambao baba yangu Daudi aliwaweka.
“Pia nitumie magogo ya mierezi, misunobari na misandali kutoka Lebanoni kwa maana najua kwamba watu wako wanao ujuzi wa kupasua mbao huko. Watu wangu watafanya kazi pamoja na watu wako ili wanipatie mbao kwa wingi kwa sababu Hekalu nitakalojenga lazima liwe kubwa na zuri kabisa. 10 Nitawapa watumishi wako, yaani maseremala wakatao mbao, kori elfu ishirini*Kori 20,000 za ngano ni sawa na lita 4,400. za unga wa ngano, kori elfu ishirini za shayiri, bathi elfu ishiriniBathi 20,000 za mvinyo au mafuta ni sawa na lita 440,000. za mvinyo, na bathi elfu ishirini za mafuta ya zeituni.”
11 Ndipo Hiramu mfalme wa Tiro akamjibu Sulemani kwa barua:
“Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawapenda watu wake, amekufanya wewe kuwa mfalme wao.”
12 Naye Hiramu akaongeza kusema:
“Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliyeziumba mbingu na nchi! Amempa Mfalme Daudi mwana mwenye hekima, aliyejaliwa maarifa na busara, ambaye atajenga Hekalu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe.
13 “Mimi nitamtuma kwako Huram-Abi, mtu mwenye ustadi mwingi, 14 ambaye mama yake alitoka Dani na baba yake alitoka Tiro. Yeye ni stadi wa kutengeneza vitu, kufanya kazi zote za dhahabu, fedha, shaba, chuma, mawe na mbao pamoja na kufuma. Ni stadi katika kutia rangi ya zambarau, buluu, nyekundu na nguo za kitani safi. Yeye ana ujuzi katika aina zote za kutia nakshi na anaweza kufuatiliza mchoro wowote wa kazi anayopewa. Atafanya kazi na mafundi wako na wale wa bwana wangu, Daudi baba yako.
15 “Sasa basi bwana wangu na awapelekee watumishi wake ngano, shayiri, mafuta ya zeituni na mvinyo kama alivyoahidi, 16 nasi tutakata magogo yote yale unayohitaji kutoka Lebanoni nasi tutayafunga pamoja na kuyaweka yaelee baharini hadi Yafa. Kisha utaweza kuyapeleka hadi Yerusalemu.”
17 Ndipo Sulemani akaamuru ifanyike hesabu ya wageni wote waliokuwa katika Israeli, baada ya ile hesabu iliyofanywa na Daudi; wakapatikana watu elfu mia moja hamsini na tatu na mia sita. 18 Akawaweka watu elfu sabini miongoni mwao kuwa wachukuzi wa mizigo, na elfu themanini kuwa wachonga mawe vilimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi ili wawahimize watu kufanya kazi.

*2:10 Kori 20,000 za ngano ni sawa na lita 4,400.

2:10 Bathi 20,000 za mvinyo au mafuta ni sawa na lita 440,000.