4
Mawakili wa siri za Mwenyezi Mungu
1 Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Al-Masihi na mawakili wa siri za Mungu. 2 Tena, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu. 3 Lakini kwangu mimi ni jambo dogo sana kwamba nihukumiwe na ninyi au na mahakama yoyote ya kibinadamu. Naam, hata mimi mwenyewe sijihukumu. 4 Dhamiri yangu ni safi, lakini hilo halinihesabii kuwa asiye na hatia. Bwana Isa ndiye anihukumuye. 5 Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni hadi Bwana Isa atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.
6 Basi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kwangu binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine. 7 Kwa maana ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na wengine? Ni nini mlicho nacho ambacho hamkupokea? Nanyi kama mlipokea, kwa nini mnajivuna kama vile hamkupokea?
8 Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi! 9 Kwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa kwenye uwanja wa tamasha, kwa sababu tumefanywa kuwa maonesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia. 10 Kwa ajili ya Al-Masihi sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Al-Masihi. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa. 11 Hadi saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao. 12 Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki; tunapoteswa, tunastahimili; 13 tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Hadi sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.
14 Siwaandikii mambo haya ili kuwaaibisha, bali ili kuwaonya, kama wanangu wapendwa. 15 Hata kama mnao walimu elfu kumi katika Al-Masihi, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Al-Masihi Isa kwa kuwaletea Injili. 16 Basi nawasihi igeni mfano wangu. 17 Kwa sababu hii ninamtuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana Isa. Yeye atawakumbusha kuhusu njia za maisha yangu katika Al-Masihi Isa, ambayo yanakubaliana na mafundisho yangu ninayofundisha katika kila kundi la waumini.
18 Baadhi yenu mmekuwa na jeuri mkidhani kuwa sitafika kwenu. 19 Lakini kama Bwana Isa akipenda, nitafika kwenu hivi karibuni, nami nitajua, si tu kile wanachosema hawa watu jeuri, bali pia nguvu yao. 20 Kwa kuwa ufalme wa Mungu si maneno matupu tu bali ni nguvu. 21 Ninyi amueni. Je, nije kwenu na fimbo, au nije kwa upendo na kwa roho ya upole?