15
Kufufuka kwa Al-Masihi
Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.
Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Al-Masihi alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama Maandiko yanavyosema, ya kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama Maandiko yanavyosema, na kwamba alimtokea Kefa*yaani Petro, kisha akawatokea wale kumi na wawili. Baadaye akawatokea wale ndugu waumini zaidi ya mia tano kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala. Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote. Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.
Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu niliwatesa waumini wa Mungu. 10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami. 11 Hivyo basi, kama ilikuwa mimi au wao, hili ndilo tunalohubiri, na hili ndilo mliloamini.
Ufufuo wa wafu
12 Basi kama tumehubiri kwamba Al-Masihi alifufuliwa kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu? 13 Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Al-Masihi hakufufuliwa. 14 Tena ikiwa Al-Masihi hakufufuliwa kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili. 15 Zaidi ya hayo, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Al-Masihi kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi. 16 Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Al-Masihi hajafufuka. 17 Tena kama Al-Masihi hajafufuliwa, imani yenu ni batili; nanyi bado mko katika dhambi zenu. 18 Hivyo basi, wote waliolala katika Al-Masihi wamepotea. 19 Ikiwa tumaini letu ndani ya Al-Masihi ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wote.
20 Lakini kweli Al-Masihi amefufuliwa kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala. 21 Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kupitia kwa mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kupitia kwa mtu mmoja. 22 Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Al-Masihi wote watafanywa hai. 23 Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Al-Masihi, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja. 24 Ndipo mwisho utafika, atakapomkabidhi Mungu BabaJina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi ufalme, baada ya kuangamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu. 25 Kwa maana lazima Al-Masihi atawale hadi awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. 26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. 27 Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake”. Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Al-Masihi hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa. 28 Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.
29 Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao? 30 Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa? 31 Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Al-Masihi Isa Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku. 32 Kama kwa sababu za kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani? Kama wafu hawafufuliwi,
“Tuleni na kunywa,
kwa kuwa kesho tutakufa.”
33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” 34 Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, wala msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.
Mwili wa ufufuo
35 Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36 Ninyi wapumbavu kiasi gani? Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa. 37 Mpandapo, hampandi mwili ule utakao kuwa, bali mwapanda mbegu tu, pengine ya ngano au ya kitu kingine. 38 Lakini Mungu huipa mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake. 39 Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti. 40 Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini fahari ya ile miili ya mbinguni ni ya aina moja, na fahari ya ile miili ya duniani ni ya aina nyingine. 41 Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.
42 Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika; 43 unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu, 44 unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho.
Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia. 45 Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima. 46 Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni. 48 Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni. 49 Kama vile tulivyochukua mfano wa mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.
50 Ndugu zangu nisemalo ni hili: mwili na damu haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika. 51 Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa: 52 ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa. 53 Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa. 54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”
55 “Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako?
Uko wapi, ee mauti, uchungu wako?”
56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini Mungu apewe shukrani, yeye atupaye ushindi kupitia kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapendwa, simameni imara. Msitikisike. Mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana Isa, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana Isa si bure.

*15:5 yaani Petro

15:24 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.