16
Changizo kwa ajili ya watakatifu
1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makundi ya waumini ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake, na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango. 3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu. 4 Ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.
Mahitaji binafsi
5 Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia. 6 Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo. 7 Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana Isa akipenda. 8 Lakini nitakaa Efeso hadi wakati wa Pentekoste, 9 kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.
10 Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana Isa, kama mimi nifanyavyo. 11 Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu.
12 Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.
Maneno ya mwisho
13 Kesheni; simameni imara katika imani; kuweni mashujaa na hodari. 14 Fanyeni kila kitu katika upendo.
15 Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio walikuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi, 16 mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii. 17 Nilifurahi Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu. 18 Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.
Salamu za mwisho
19 Makundi ya waumini wa jimbo la Asia wanawasalimu.
Akila na Prisila*kwa Kiyunani ni Priska pamoja na kundi la waumini walioko nyumbani mwao wanawasalimu sana katika Bwana Isa.
20 Ndugu wote walio hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
21 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.
22 Kama mtu yeyote hampendi Bwana Isa Al-Masihi, na alaaniwe. Bwana wetu Isa, njoo†kwa Kiaramu ni Marana tha.
23 Neema ya Bwana Isa iwe nanyi.
24 Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Al-Masihi Isa. Amen.