2 Wakorintho
1
Salamu
Barua hii ni kutoka kwangu mimi Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu.
Kwa kundi la waumini wa Mungu walioko Korintho, pamoja na watakatifu wote walio nchi ya Akaya yote.
Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba*Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
Mungu wa faraja yote
Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. Kama vile mateso ya Al-Masihi yanavyozidi maishani mwetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kupitia kwa Al-Masihi. Ikiwa tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki faraja yetu.
Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko jimbo la Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi. Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. 10 Yeye ametuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo, na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa, 11 kama vile mnavyoungana kusaidiana nasi katika maombi. Hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.
Paulo aahirisha ziara
12 Basi haya ndio majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeishi katika ulimwengu kwa utakatifu na uaminifu unaotoka kwa Mungu, na hasa katika uhusiano wetu na ninyi. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu. 13 Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba, 14 kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Isa.
15 Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia, na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Yudea. 17 Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kwa hali ya mwili, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo?
18 Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajakuwa “Ndiyo” na “Siyo”. 19 Kwa kuwa Isa Al-Masihi, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silvanoyaani Sila, na Timotheo tulimhubiri kwenu, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo”, bali kwake yeye siku zote ni “Ndiyo”. 20 Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Al-Masihi ni “Ndiyo”. Kwa sababu hii, ni kwake yeye tunasema “Amen” kwa utukufu wa Mungu. 21 Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Al-Masihi. Alitupaka mafuta 22 kwa kututia muhuri wake na kutupatia Roho wake Mtakatifu mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia yote aliyotuahidi.
23 Namwita Mungu awe shahidi wangu kwamba sikurudi Korintho kwa sababu niliwahurumia ninyi. 24 Si kwamba tunatawala imani yenu, bali twatenda kazi pamoja nanyi ili mfurahi, kwa sababu ni kwa imani mwasimama imara.

*1:2 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.

1:19 yaani Sila