2
1 Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi. 2 Kwa kuwa nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha? 3 Niliwaandikia hivyo ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao walipaswa kunifurahisha. Nilikuwa na uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu. 4 Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana moyoni mwangu, tena kwa machozi mengi; shabaha yangu haikuwa niwahuzunishe, bali niwaoneshe kina cha upendo wangu kwenu.
Msamaha kwa mwenye dhambi
5 Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote. Nasema hivi ili nisiwe mkali kupita kiasi. 6 Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha. 7 Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi. 8 Kwa hiyo, nawasihi mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwake. 9 Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo. 10 Mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Al-Masihi kwa ajili yenu, 11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatujakosa kuzijua hila zake.
Wasiwasi wa Paulo huko Troa
12 Basi nilipofika Troa kuhubiri Injili ya Al-Masihi na kukuta kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa amenifungulia mlango, 13 bado nilikuwa sina amani kwa sababu sikumkuta ndugu yangu Tito huko. Hivyo niliagana nao, nikaenda Makedonia.
14 Lakini Mungu apewe shukrani, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Al-Masihi. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye. 15 Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Al-Masihi miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea. 16 Kwa wale wanaopotea, sisi ni harufu ya mauti iletayo mauti; lakini kwa wale wanaookolewa, sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo? 17 Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na neno la Mungu ili tujifaidishe. Bali tunalinena neno lake kwa unyofu katika Al-Masihi tukiwa mbele za Mungu, kama watu waliotumwa na Mungu.