3
Wahudumu wa agano jipya
1 Je, tunaanza tena kujisifu wenyewe? Au tunahitaji kupata barua za utambulisho kwenu au kutoka kwenu, kama watu wengine? 2 Ninyi wenyewe ndio barua yetu iliyoandikwa katika mioyo yetu, inayojulikana na kusomwa na kila mtu. 3 Nanyi mwadhihirisha wazi kwamba ninyi ni barua inayotoka kwa Al-Masihi, matokeo ya huduma yetu, ambayo haikuandikwa kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai, si katika vibao vya mawe, bali katika vibao ambavyo ni mioyo ya wanadamu.
4 Hili ndilo tumaini tulilo nalo mbele za Mungu kupitia kwa Al-Masihi. 5 Si kwamba sisi tunafikiri kuwa tunaweza kufanya jambo lolote wenyewe, lakini utoshelevu wetu unatoka kwa Mungu. 6 Ndiye alitutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya: si wa andiko, bali wa Roho wa Mungu; kwa kuwa andiko huua, bali Roho hutia uzima.
Utukufu wa agano jipya
7 Basi ikiwa ile huduma iliyoleta mauti, iliyoandikwa kwa herufi juu ya jiwe, ilikuja kwa utukufu hata Waisraeli wakawa hawawezi kuutazama uso wa Musa kwa sababu ya ule utukufu wake, ingawa ulikuwa wa kufifia, 8 je, huduma ya Roho wa Mungu haitakuwa na utukufu zaidi? 9 Ikiwa huduma ile inayowahukumu wanadamu ina utukufu, je, ile huduma iletayo haki haitakuwa ya utukufu zaidi? 10 Kwa maana kile kilichokuwa na utukufu sasa hakina utukufu, kikilinganishwa na huu utukufu unaozidi. 11 Ikiwa kile kilichokuwa kinafifia kilikuja kwa utukufu, je, si zaidi utukufu wa kile kinachodumu!
12 Kwa hiyo, kwa kuwa tunalo tumaini hili, tuna ujasiri sana. 13 Sisi si kama Musa, ambaye ilimpasa kuweka utaji wa kufunika uso wake ili Waisraeli wasiuone ule mng’ao uliokuwa juu yake hadi ulipofifia na hatimaye kutoweka. 14 Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana hadi leo utaji ule ule hufunika Torati inaposomwa. Huo utaji haujaondolewa, kwa maana ni katika Al-Masihi peke yake unaondolewa. 15 Hata leo Torati ya Musa inaposomwa, utaji hufunika mioyo yao. 16 Lakini wakati wowote mtu anapomgeukia Bwana Mungu Mwenyezi, utaji unaondolewa. 17 Basi Bwana Isa ndiye Roho. Mahali alipo Roho wa Bwana Mungu Mwenyezi, hapo pana uhuru. 18 Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji, tunadhihirisha utukufu wa Bwana Isa kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu mkuu zaidi, unaotoka kwa Bwana Isa, aliye Roho.