14
Unabii wa Ahiya dhidi ya Yeroboamu
1 Wakati ule, Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua, 2 naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme wa watu hawa, yuko huko. 3 Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.” 4 Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama mumewe alivyosema, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo.
Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake. 5 Lakini Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.”
6 Hivyo, Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini unajifanya kuwa si wewe? Nimetumwa kwako kukupa habari mbaya. 7 Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli. 8 Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu. 9 Umefanya maovu mengi kuliko wote waliokutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunigeuka.
10 “ ‘Kwa sababu hii, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu hadi iteketee yote kama mtu anavyochoma kinyesi. 11 Mbwa watawala walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani. Mwenyezi Mungu amenena!’
12 “Lakini wewe, rudi nyumbani. Utakapofika mji wako, kijana atakufa. 13 Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Ni yeye pekee wa nyumba ya Yeroboamu atakayezikwa, kwa sababu ni yeye tu ndani ya nyumba ya Yeroboamu ambaye Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ameona kitu chema kwake.
14 “Mwenyezi Mungu atajiinulia mwenyewe mfalme juu ya Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Siku hiyo itakuwa lini? Hata sasa yameanza kutokea. 15 Naye Mwenyezi Mungu ataipiga Israeli, hata iwe kama mwanzi unaoyumbayumba kwenye maji. Ataing’oa Israeli kutoka nchi hii nzuri aliyowapa baba zao na kuwatawanya ng’ambo ya Mto*yaani Mto Frati, kwa sababu wamemghadhibisha Mwenyezi Mungu kwa kutengeneza nguzo za Ashera. 16 Naye atawaacha Israeli kwa sababu ya dhambi Yeroboamu alizozitenda na kuisababisha Israeli kuzitenda.”
17 Kisha, mke wa Yeroboamu akainuka, akaondoka kwenda Tirsa. Mara alipokanyaga kizingiti cha mlango, kijana akafa. 18 Wakamzika na Israeli yote ikamwombolezea, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema kupitia kwa mtumishi wake, nabii Ahiya.
19 Matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, vita vyake na jinsi alivyotawala, vimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. 20 Yeroboamu akawatawala kwa miaka ishirini na mbili, kisha akalala na baba zake. Naye Nadabu mwanawe akawa mfalme baada yake.
Rehoboamu mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 11:5–12:15)
21 Rehoboamu mwana wa Sulemani alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kuwa mfalme, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi Mungu alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, na alikuwa Mwamoni.
22 Yuda wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu kuliko baba zao walivyofanya. 23 Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia, mawe ya kuabudiwa, na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda. 24 Kulikuwa na hata mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi. Watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli.
25 Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu. 26 Akachukua hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao zote za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa amezitengeneza. 27 Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. 28 Kila wakati mfalme alipoenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, walinzi walizichukua hizo ngao, na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.
29 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 30 Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. 31 Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama; alikuwa Mwamoni. Naye Abiya†au Abiyamu mwanawe akawa mfalme baada yake.