15
Abiya mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 13:1–14:1)
1 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya akawa mfalme wa Yuda, 2 naye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka binti Abishalomu*yaani Absalomu.
3 Alitenda dhambi zote baba yake alizotenda kabla yake; moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake ulivyokuwa. 4 Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi, Mwenyezi Mungu, Mungu wake, akampa taa katika Yerusalemu kwa kumwinua mwana atawale baada yake ili kuifanya Yerusalemu kuwa imara. 5 Kwa kuwa Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, wala hakushindwa kuzishika amri zote za Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yake, isipokuwa kwa suala la Uria, Mhiti.
6 Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu wakati wote wa maisha ya Abiya. 7 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Abiya na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu. 8 Naye Abiya akalala na baba zake akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake.
Asa mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 15:16–16:6)
9 Katika mwaka wa ishirini wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa akawa mfalme wa Yuda, 10 naye akatawala katika Yerusalemu miaka arobaini na moja. Bibi yake aliitwa Maaka binti Abishalomu.
11 Asa akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama alivyokuwa ametenda Daudi, baba yake. 12 Akawafukuza mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu kutoka nchi, na kuondoa sanamu zote ambazo baba zake walikuwa wametengeneza. 13 Hata akamwondoa bibi yake Maaka kwenye wadhifa wake kama mama malkia, kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni. 14 Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Mwenyezi Mungu kikamilifu maisha yake yote. 15 Akaleta ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu fedha na dhahabu na vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.
16 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha, mfalme wa Israeli siku zote za utawala wao. 17 Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome katika mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia katika nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.
18 Kisha Asa akachukua fedha yote na dhahabu zilizokuwa zimeachwa katika hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika jumba lake la kifalme. Kisha akawakabidhi maafisa wake na kuwatuma kwa Ben-Hadadi mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Aramu†yaani Shamu, aliyekuwa akitawala Dameski. 19 Akasema, “Na tufanye mkataba kati yangu na wewe, kama ilivyokuwa kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea zawadi ya fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha, mfalme wa Israeli ili aniondokee.”
20 Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Akaishinda miji ya Iyoni, Dani, Abel-Beth-Maaka na Kinerethi yote, pamoja na Naftali. 21 Baasha aliposikia jambo hili, akasimamisha ujenzi wa Rama, akaenda kuishi Tirsa. 22 Kisha Mfalme Asa akatoa amri kwa Yuda yote, pasipo kumwacha hata mmoja, kubeba mawe na mbao kutoka Rama, ambazo Baasha alikuwa akizitumia huko. Mfalme Asa akazitumia kujengea Geba iliyo Benyamini na Mispa.
23 Kwa matukio yote ya utawala wa Asa, mafanikio yake yote, yote aliyofanya na miji aliyoijenga, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Hata hivyo, katika uzee wake alishikwa na ugonjwa wa miguu. 24 Kisha Asa akalala na baba zake, naye akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake.
Nadabu mfalme wa Israeli
25 Nadabu mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika mwaka wa pili wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, naye akatawala Israeli kwa miaka miwili. 26 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akienenda katika njia za baba yake na katika dhambi yake, aliyoisababisha Israeli kutenda.
27 Baasha mwana wa Ahiya wa nyumba ya Isakari akapanga njama dhidi ya Nadabu, naye akamuua huko Gibethoni, mji wa Wafilisti, wakati Nadabu na Israeli yote walikuwa wameuzingira. 28 Baasha akamuua Nadabu katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, naye Baasha akawa mfalme baada yake.
29 Mara tu alipoanza kutawala, aliwaua watu wote wa nyumba ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu hata mtu mmoja akiwa hai, bali aliwaangamiza wote, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu kupitia kwa mtumishi wake Ahiya Mshiloni. 30 Haya yalitendeka kwa sababu ya dhambi alizozitenda Yeroboamu, zilizosababisha Israeli kutenda dhambi, na kwa sababu alimkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
31 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Nadabu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
32 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli wakati wote wa utawala wao.
Baasha mfalme wa Israeli
33 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya akawa mfalme wa Israeli yote huko Tirsa, naye akatawala kwa miaka ishirini na nne. 34 Akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akienenda katika njia ya Yeroboamu na dhambi yake, aliyosababisha Israeli kuitenda.