16
21 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yehu mwana wa Hanani dhidi ya Baasha, kusema: “Nilikuinua kutoka mavumbini na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli, lakini ukaenenda katika njia za Yeroboamu na kusababisha watu wangu Israeli kutenda dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao. Basi nitamwangamiza Baasha pamoja na nyumba yake, nami nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwanawe Nebati. Mbwa watawala walio wa nyumba ya Baasha watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani.”
Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Baasha, aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Baasha akalala na baba zake naye akazikwa huko Tirsa. Naye Ela mwanawe akawa mfalme baada yake.
Zaidi ya hayo, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Baasha pamoja na nyumba yake kupitia kwa nabii Yehu mwana wa Hanani, kwa sababu ya maovu yote aliyokuwa ametenda machoni pa Mwenyezi Mungu, akimkasirisha kwa mambo aliyotenda, na kuwa kama nyumba ya Yeroboamu aliyoiangamiza.
Ela mfalme wa Israeli
Katika mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala huko Tirsa kwa miaka miwili.
Zimri, mmoja wa maafisa wake, aliyekuwa na amri juu ya nusu ya magari yake ya vita, akapanga njama dhidi ya Ela. Wakati huo Ela alikuwa Tirsa, akilewa katika nyumba ya Arsa, aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme huko Tirsa. 10 Zimri akaingia, akampiga na kumuua katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Kisha Zimri akawa mfalme baada yake.
11 Mara tu alipoanza kutawala na kukalia kiti chake cha kifalme, aliua jamaa yote ya Baasha. Hakumwacha mwanaume hata mmoja, akiwa ni ndugu au rafiki. 12 Hivyo, Zimri akawaangamiza jamaa yote ya Baasha, kama Mwenyezi Mungu alivyonena dhidi ya Baasha kupitia kwa nabii Yehu: 13 kwa sababu ya dhambi zote Baasha na mwanawe Ela walizokuwa wametenda na wakasababisha Israeli kuzitenda, basi wakamkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sanamu zao batili.
14 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ela, na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Zimri mfalme wa Israeli
15 Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala huko Tirsa siku saba. Jeshi lilikuwa limepiga kambi karibu na Gibethoni, mji wa Wafilisti. 16 Waisraeli waliokuwa kambini waliposikia kuwa Zimri amepanga njama ya kumuua mfalme, wakamtangaza Omri, jemadari wa jeshi, kuwa mfalme wa Israeli yote siku hiyo hiyo huko kambini. 17 Ndipo Omri na Waisraeli wote pamoja naye wakaondoka Gibethoni na kuizingira Tirsa. 18 Zimri alipoona kuwa mji umechukuliwa, alienda ndani ya ngome ya jumba la kifalme na kulichoma moto hilo jumba na kujiteketeza ndani yake. Kwa hiyo akafa, 19 kwa sababu ya dhambi alizotenda, akifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu na kuenenda katika njia za Yeroboamu na katika dhambi alizotenda na kusababisha Israeli kuzifanya.
20 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Zimri, na uasi alioutenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Omri mfalme wa Israeli
21 Kisha, watu wa Israeli wakagawanyika katika makundi mawili, nusu wakamuunga mkono Tibni mwana wa Ginathi ili awe mfalme, na nusu nyingine wakamuunga mkono Omri. 22 Lakini wafuasi wa Omri wakajionesha kuwa wenye nguvu kuliko wale wa Tibni, mwana wa Ginathi. Hivyo Tibni akafa, na Omri akawa mfalme.
23 Katika mwaka wa thelathini na moja wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala kwa miaka kumi na mbili, sita kati ya hiyo katika Tirsa. 24 Alinunua kilima cha Samaria kutoka kwa Shemeri kwa talanta mbili*Talanta 2 za fedha ni sawa na kilo 70. za fedha na akajenga mji juu ya hicho kilima, akiuita Samaria, kutokana na Shemeri, jina la mmiliki wa kwanza wa kilima hicho.
25 Lakini Omri akatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu na kutenda dhambi kuliko wote waliomtangulia. 26 Akaenenda katika njia zote za Yeroboamu mwana wa Nebati na katika dhambi zake, ambazo alisababisha Israeli kutenda, hivyo basi wakamkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sanamu zao batili.
27 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Omri, yale aliyofanya na mafanikio aliyokuwa nayo, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 28 Omri akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Ahabu mwanawe akawa mfalme baada yake.
Ahabu afanywa mfalme wa Israeli
29 Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala Israeli akiwa Samaria kwa miaka ishirini na mbili. 30 Ahabu mwana wa Omri akafanya maovu zaidi machoni pa Mwenyezi Mungu kuliko yeyote aliyemtangulia. 31 Kama vile haikutosha kuishi kama Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, naye akaanza kumtumikia Baali na kumwabudu. 32 Akatengeneza madhabahu kwa ajili ya Baali katika hekalu la Baali alilolijenga huko Samaria. 33 Pia Ahabu alitengeneza nguzo ya Ashera na kufanya mengi ili kumkasirisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuliko walivyofanya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia.
34 Wakati wa Ahabu, Hieli ule Mbetheli, akaijenga Yeriko upya. Aliweka misingi yake kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, na kuweka malango yake kwa gharama ya mwanawe mdogo Segubu, kama Mwenyezi Mungu alivyonena kupitia kwa Yoshua, mwana wa Nuni.

*16:24 Talanta 2 za fedha ni sawa na kilo 70.