17
Ilya atangaza ukame
Basi Ilya Mtishbi, kutoka Tishbi katika Gileadi, akamwambia Ahabu, “Kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli ninayemtumikia, aishivyo, hapatakuwa na umande wala mvua katika miaka kadhaa ijayo, isipokuwa kwa neno langu.”
Ilya alishwa na kunguru
Kisha neno la Mwenyezi Mungu likamjia Ilya, kusema, “Ondoka hapa, elekea upande wa mashariki ukajifiche karibu na Kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yordani. Utakunywa maji kutoka kile kijito, nami nimeagiza kunguru wakulishe huko.”
Naye akafanya kama alivyoambiwa na Mwenyezi Mungu. Akaenda katika Kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yordani na akakaa huko. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, naye akanywa maji kutoka kile kijito.
Baada ya muda, kile kijito kikakauka kwa sababu mvua haikuwa imenyesha katika nchi.
Ilya na mjane wa Sarepta
Kisha neno la Mwenyezi Mungu likamjia Ilya, kusema, “Ondoka, uende Sarepta ya Sidoni, ukae huko. Nimemwagiza mjane wa huko ili akuhudumie.” 10 Hivyo akaenda Sarepta. Alipofika kwenye lango la mji, alimkuta mjane akiokota kuni pale. Akamwita na kumwambia, “Naomba uniletee maji kidogo kwenye gudulia ili niweze kunywa.” 11 Alipokuwa anaenda kumletea, akamwita akasema, “Tafadhali niletee pia kipande cha mkate.”
12 Akamjibu, “Hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aishivyo, sina mkate wowote, isipokuwa konzi moja ya unga kwenye chungu, na mafuta kidogo kwenye chupa. Ninakusanya kuni chache nipeleke nyumbani na nikapike chakula kwa ajili yangu na mwanangu, ili tule, kiishe, tukafe.”
13 Ilya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mkate mdogo kutoka vile ulivyo navyo kisha uniletee na ndipo utayarishe chochote kwa ajili yako na mwanao. 14 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Kile chungu cha unga hakitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile Mwenyezi Mungu atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ”
15 Akaondoka na kufanya kama Ilya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Ilya, yule mwanamke na jamaa yake. 16 Kwa kuwa kile chungu hakikuisha unga na ile chupa ya mafuta haikukauka sawasawa na lile neno la Mwenyezi Mungu lililonenwa na Ilya.
17 Baada ya muda, mwana wa yule mwanamke mwenye nyumba akaugua. Hali yake ikaendelea kuwa mbaya sana, na hatimaye akaacha kupumua. 18 Yule mjane akamwambia Ilya, “Una nini dhidi yangu, ewe mtu wa Mungu? Umekuja ili kunikumbusha dhambi yangu, na kusababisha kifo cha mwanangu?”
19 Ilya akamjibu, “Nipe mwanao.” Ilya akampokea kutoka kifuani mwake, akambeba hadi chumba cha juu alipokuwa anaishi, akamlaza kitandani pake. 20 Kisha akamlilia Mwenyezi Mungu, akasema “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, je, pia umeleta msiba juu ya mjane huyu ninayeishi kwake, kwa kusababisha mwanawe kufa?” 21 Kisha akajinyoosha juu ya kijana mara tatu na kumlilia Mwenyezi Mungu, akisema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nakuomba roho ya huyu kijana imrudie!”
22 Mwenyezi Mungu akasikia kilio cha Ilya, na roho ya kijana ikamrudia, naye akafufuka. 23 Ilya akamtwaa kijana na kumbeba kutoka chumba chake cha juu, akamshusha, akampa mama yake na kusema, “Tazama, mwanao yu hai!”
24 Ndipo yule mwanamke akamwambia Ilya, “Sasa ninajua kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na kwamba neno la Mwenyezi Mungu kutoka kinywani mwako ni kweli.”