18
Ilya na Obadia
1 Baada ya muda mrefu, katika mwaka wa tatu, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Ilya kusema, “Nenda ukajioneshe kwa Ahabu nami nitaleta mvua juu ya nchi.” 2 Kwa hiyo Ilya akaenda kujionesha kwa Ahabu.
Wakati huo njaa ilikuwa kali sana katika Samaria, 3 naye Ahabu alikuwa amemwita Obadia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme. (Obadia alimcha Mwenyezi Mungu sana. 4 Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Mwenyezi Mungu, Obadia alikuwa amewachukua manabii mia moja na kuwaficha katika mapango mawili, hamsini kwenye kila moja, na akawa akiwapa chakula na maji.) 5 Ahabu alikuwa amemwambia Obadia, “Nenda katika nchi yote kwenye vijito vyote na mabonde. Huenda tunaweza kupata majani ya kuwalisha farasi na nyumbu ili wapate kuishi, tusilazimike kumuua hata mmoja wa wanyama wetu.” 6 Kwa hiyo wakagawanya nchi waliyokusudia kutafuta majani, Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.
7 Obadia alipokuwa akitembea njiani, Ilya akakutana naye. Obadia akamtambua, akasujudu, uso wake ukigusa chini, na kusema, “Je, hivi kweli ni wewe, bwana wangu Ilya?”
8 Ilya akamjibu, “Ndiyo, nenda ukamwambie bwana wako, ‘Ilya yuko hapa.’ ”
9 Obadia akamuuliza, “Ni kosa gani nimefanya, hata ukaamua kumkabidhi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu ili aniue? 10 Hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aishivyo, hakuna taifa hata moja au ufalme ambapo bwana wangu hajamtuma mtu kukutafuta. Kila wakati taifa au ufalme walipodai kwamba haupo huko, aliwafanya waape kwamba hawakuweza kukupata. 11 Lakini sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kusema, ‘Ilya yuko hapa.’ 12 Sijui ni wapi Roho wa Mwenyezi Mungu ataamua kukupeleka wakati nitakapokuacha. Nikienda kumwambia Ahabu na asikupate, ataniua; lakini mimi mtumishi wako nimekuwa nikimwabudu Mwenyezi Mungu tangu ujana wangu. 13 Je, hukusikia, bwana wangu, nilifanya nini Yezebeli alipokuwa akiua manabii wa Mwenyezi Mungu? Niliwaficha manabii wa Mwenyezi Mungu mia moja katika mapango mawili, hamsini katika kila moja, na nikawapatia chakula na maji. 14 Nawe sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kumwambia, ‘Ilya yuko hapa.’ Yeye ataniua!”
15 Ilya akasema, “Kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni aishivyo, yeye ninayemtumikia, hakika nitajionesha kwa Ahabu leo.”
Ilya juu ya Mlima Karmeli
16 Basi Obadia akaenda kukutana na Ahabu na kumwambia; naye Ahabu akaenda kukutana na Ilya. 17 Ahabu alipomwona Ilya, akamwambia, “Je, ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?”
18 Ilya akamjibu, “Mimi sijaitaabisha Israeli. Lakini wewe na jamaa ya baba yako ndio mnaofanya hivyo. Mmeziacha amri za Mwenyezi Mungu na mkafuata Mabaali. 19 Sasa waite watu kutoka Israeli yote tukutane nao juu ya Mlima Karmeli. Nawe uwalete hao manabii wa Baali mia nne na hamsini na hao manabii mia nne wa Ashera, walao chakula mezani mwa Yezebeli.”
20 Ndipo Ahabu akatuma ujumbe katika Israeli yote na kuwakusanya manabii hao juu ya Mlima Karmeli. 21 Ilya akasimama mbele ya watu na kusema, “Mtayumbayumba katikati ya mawazo mawili hadi lini? Ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu, mfuateni yeye; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye.”
Lakini watu hawakusema kitu.
22 Kisha Ilya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa Mwenyezi Mungu aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini. 23 Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na wamweke juu ya kuni, lakini wasimwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni, lakini sitamwashia moto. 24 Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la Mwenyezi Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.”
Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.”
25 Ilya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.” 26 Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa.
Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga.
27 Wakati wa adhuhuri, Ilya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.” 28 Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja kwa visu na vyembe, hadi damu ikachuruzika. 29 Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu hadi wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na itikio, hakuna aliyejibu, na hakuna aliyezingatia.
30 Kisha Ilya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Wakamkaribia, naye akaikarabati madhabahu ya Mwenyezi Mungu, iliyokuwa imeharibiwa. 31 Ilya akachukua mawe kumi na mbili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la Mwenyezi Mungu lilimjia, kusema, “Jina lako litakuwa Israeli.” 32 Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la Mwenyezi Mungu, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu. 33 Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.”
34 Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena.
Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu. 35 Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki.
36 Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Ilya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kama ulivyoagiza. 37 Unijibu, Ee Mwenyezi Mungu! Unijibu ili watu hawa wajue kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”
38 Kisha moto wa Mwenyezi Mungu ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.
39 Watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Mwenyezi Mungu: yeye ndiye Mungu! Mwenyezi Mungu: yeye ndiye Mungu!”
40 Kisha Ilya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Ilya akawaleta Bonde la Kishoni na kuwachinja huko.
41 Ilya akamwambia Ahabu, “Nenda, ukale na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.” 42 Hivyo Ahabu akaondoka ili kula na kunywa. Lakini Ilya akapanda kileleni mwa Karmeli, akainama hadi chini, na kuweka kichwa chake katikati ya magoti.
43 Akamwambia mtumishi wake, “Nenda ukatazame kuelekea bahari.” Akaenda na kutazama.
Akasema, “Hakuna kitu chochote huko.”
Mara saba Ilya akasema, “Nenda tena.”
44 Mara ya saba, mtumishi akaleta taarifa, “Wingu dogo kama mkono wa mwanadamu linainuka kutoka baharini.”
Hivyo Ilya akasema, “Nenda ukamwambie Ahabu, ‘Tandika gari lako la vita, ushuke kabla mvua haijakuzuia.’ ”
45 Wakati ule ule anga likawa jeusi kwa mawingu, upepo ukainuka na mvua kubwa ikanyesha, naye Ahabu akaenda zake Yezreeli. 46 Nguvu za Mwenyezi Mungu zikamjia Ilya, naye akajikaza viuno, akakimbia mbele ya Ahabu njia yote hadi ingilio la Yezreeli.