19
Ilya akimbilia Horebu
1 Ahabu akamwambia Yezebeli kila kitu Ilya alichokuwa amefanya na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga. 2 Hivyo Yezebeli akamtuma mjumbe kwa Ilya, kusema, “Miungu waniadhibu vikali zaidi, ikiwa kesho wakati kama huu sitakuwa nimeondoa uhai wako kama mmoja wa hao manabii.”
3 Ilya aliogopa, na akatoroka kuokoa maisha yake. Alipofika Beer-Sheba katika Yuda, akamwacha mtumishi wake huko, 4 lakini yeye mwenyewe akatembea mwendo wa kutwa nzima katika jangwa. Akafika kwenye mti wa mretemu, akakaa chini yake na kuomba ili afe. Akasema, “Yatosha sasa, Mwenyezi Mungu, ondoa roho yangu, kwani mimi si bora kuliko baba zangu.” 5 Kisha akajinyoosha chini ya mti, akalala usingizi.
Mara malaika akamgusa na kumwambia, “Inuka ule.” 6 Akatazama pande zote, na hapo karibu na kichwa chake palikuwa na mkate uliookwa kwenye makaa ya moto, na gudulia la maji. Akala na kunywa, kisha akajinyoosha tena.
7 Yule malaika wa Mwenyezi Mungu akaja tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Inuka ule, kwa kuwa bado una safari ndefu mbele yako.” 8 Kwa hiyo akainuka, akala na kunywa. Akiwa ametiwa nguvu na kile chakula, akasafiri siku arobaini usiku na mchana hadi akafika Horebu, mlima wa Mungu. 9 Huko akaingia katika pango, akalala humo usiku ule.
Mwenyezi Mungu amtokea Ilya
Nalo neno la Mwenyezi Mungu likamjia, kusema, “Unafanya nini hapa, Ilya?”
10 Akajibu, “Nimekuwa nikifanya bidii sana kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Waisraeli wamelikataa agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi peke yangu niliyebaki, sasa wananitafuta ili waniue pia.” 11 Mwenyezi Mungu akasema, “Toka nje ukasimame juu ya mlima mbele za Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu yu karibu kupita hapo.”
Kisha upepo mzito na wenye nguvu ukapasua milima ile na kuvunjavunja miamba mbele za Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo katika ule upepo. Baada ya upepo palikuwa na tetemeko la ardhi, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo kwenye lile tetemeko. 12 Baada ya tetemeko la ardhi moto ukaja, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo katika ule moto. Baada ya moto ikaja sauti ya utulivu ya kunong’ona. 13 Ilya alipoisikia, akafunika uso kwa vazi lake, akatoka na kusimama kwenye mlango wa pango.
Kisha ile sauti ikamwambia, “Ilya, unafanya nini hapa?”
14 Akajibu, “Nimekuwa nikifanya bidii sana kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Waisraeli wamelikataa agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi peke yangu niliyebaki, sasa wananitafuta ili waniue pia.”
15 Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Utakapofika huko, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu*yaani Shamu. 16 Pia mpake mafuta Yehu, mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umpake mafuta Al-Yasa mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola awe nabii baada yako. 17 Yehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Al-Yasa atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu. 18 Hata sasa nimeweka akiba ya watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.”
Wito wa Al-Yasa
19 Hivyo Ilya akaondoka huko na kumkuta Al-Yasa mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliiongoza ile jozi ya kumi na mbili. Ilya akamwendea, na kumvisha vazi lake. 20 Kisha Al-Yasa akawaacha maksai wake, akamkimbilia Ilya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.”
Ilya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekufanya nini?”
21 Basi Al-Yasa akamwacha Ilya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Ilya, akamtumikia.