20
Ben-Hadadi aishambulia Samaria
Basi, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira Samaria na kuishambulia kwa jeshi. Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Fedha yako na dhahabu yako ni vyangu; nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’ ”
Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.”
Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimewatuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako. Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’ ”
Mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi, akawaambia, “Tazama jinsi mtu huyu anavyochochea matatizo! Alipotuma apelekewe wake zangu na watoto wangu, fedha zangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.”
Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.”
Kwa hiyo akawajibu wajumbe wa Ben-Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme, ‘Mtumishi wako atafanya yote uliyoyadai mwanzoni, lakini dai hili la sasa siwezi kulitekeleza.’ ” Wakaondoka na kupeleka jibu kwa Ben-Hadadi.
10 Kisha Ben-Hadadi akatuma ujumbe mwingine kwa Ahabu, kusema, “Miungu waniadhibu vikali zaidi ikiwa vumbi la Samaria litatosheleza konzi moja ya kila mtu ya wale wanaofuatana nami.”
11 Mfalme wa Israeli akajibu, “Mwambieni, ‘Yule anayevaa mavazi ya vita asije akajisifu kama yule anayevua.’ ”
12 Ben-Hadadi alisikia ujumbe huu wakati yeye na wafalme walikuwa wakinywa katika mahema yao, akawaamuru watu wake, “Jiandaeni kushambulia.” Kwa hiyo wakajiandaa kushambulia mji.
Ahabu amshinda Ben-Hadadi
13 Wakati huo huo nabii akamjia Ahabu, mfalme wa Israeli na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Je, unaona jeshi hili kubwa? Nitalitia mkononi mwako leo, nawe utajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
14 Ahabu akauliza, “Ni nani atakayefanya hili?”
Nabii akamjibu, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Maafisa vijana majemadari wa majimbo watafanya hili.’ ”
Akauliza, “Ni nani atakayeanzisha vita?”
Nabii akamjibu, “Ni wewe.”
15 Hivyo, Ahabu akawaita maafisa vijana wapatao mia mbili thelathini na wawili (232) waliokuwa chini ya majemadari wa majimbo. Kisha akawakusanya Waisraeli waliobaki, ambao idadi yao walikuwa elfu saba. 16 Wakaondoka wakati wa adhuhuri, Ben-Hadadi na wale wafalme thelathini na wawili walioungana naye walipokuwa katika mahema yao wakilewa. 17 Maafisa vijana majemadari wa majimbo waliondoka kwanza.
Wakati huu Ben-Hadadi alikuwa amewatuma wapelelezi, ambao walileta taarifa kusema kwamba, “Askari wanasonga mbele kutoka Samaria.”
18 Akasema, “Ikiwa wamekuja kwa amani, wakamate wakiwa hai; ikiwa wamekuja kwa vita, wakamate wakiwa hai.”
19 Wale maafisa vijana majemadari wa majimbo wakatoka nje ya mji jeshi likiwa nyuma yao, 20 kila mmoja akamuua adui yake. Hii ilisababisha Waaramu kukimbia, huku Waisraeli wakiwafuatia. Lakini Ben-Hadadi, mfalme wa Aramu akapanda farasi na kutoroka pamoja na baadhi ya wapanda farasi wake. 21 Mfalme wa Israeli akasonga mbele, akawashinda farasi na magari ya vita ya adui, na kuwasababishia Waaramu hasara kubwa.
22 Baadaye nabii akaja kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Jiandae vizuri ufikirie la kufanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Aramu atakuja tena kukushambulia.”
23 Wakati huo, maafisa wa mfalme wa Aramu wakamshauri, wakamwambia, “Miungu yao ni miungu ya vilimani. Ndiyo sababu walikuwa na nguvu sana kutuzidi. Lakini tukipigana nao katika nchi tambarare, hakika tutawashinda. 24 Fanya hivi: Waondoe hao wafalme wote kutoka nafasi zao na uweke maafisa wengine mahali pao. 25 Ni lazima pia uandae jeshi lingine kama lile ulilopoteza, farasi kwa farasi, gari la vita kwa gari la vita, ili tuweze kupigana na Israeli katika nchi tambarare. Kisha kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.” Akakubaliana nao naye akashughulika ipasavyo.
26 Mwaka uliofuata, majira kama hayo, Ben-Hadadi akawakusanya Waaramu, akaenda Afeki kupigana dhidi ya Israeli. 27 Baada ya Waisraeli kukusanywa na kupewa mahitaji, walienda kukabiliana nao. Waisraeli wakapiga kambi mkabala nao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, Waaramu wakiwa wameenea katika nchi.
28 Yule mtu wa Mungu akaja na kumwambia mfalme wa Israeli, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Kwa sababu Waaramu wanafikiri Mwenyezi Mungu ni Mungu wa vilimani na sio Mungu wa mabondeni, nitalitia jeshi hili kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
29 Kwa siku saba walipiga kambi wakitazamana, na siku ya saba vita vikaanza. Waisraeli wakawajeruhi askari wa miguu wa Waaramu wapatao elfu mia moja kwa siku moja. 30 Waliobaki walikimbilia mji wa Afeki ambako elfu ishirini na saba kati yao waliangukiwa na ukuta. Naye Ben-Hadadi alikimbilia mjini na kujificha kwenye chumba cha ndani.
31 Maafisa wake wakamwambia, “Tazama, tumesikia kwamba wafalme wa nyumba ya Israeli wana huruma. Twendeni kwa mfalme wa Israeli tukiwa tumevaa gunia viunoni mwetu na kamba kuzunguka vichwa vyetu. Huenda akakuacha hai.”
32 Wakiwa wamevaa magunia viunoni mwao na kamba kuzunguka vichwa vyao, wakaenda kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Mtumishi wako Ben-Hadadi anasema: ‘Tafadhali, naomba uniache hai.’ ”
Mfalme akajibu, “Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu.”
33 Wale watu wakalipokea jambo lile kama dalili nzuri nao wakawa wepesi kulichukua neno lake wakisema, “Ndiyo, yeye ni ndugu yako Ben-Hadadi!”
Mfalme akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ikawa Ben-Hadadi alipokuja, Ahabu akampandisha katika gari lake la vita.
Ben-Hadadi akajitolea, akisema, 34 “Nitairudisha miji ambayo baba yangu aliiteka kutoka kwa baba yako. Nawe utaweka mitaa yako katika Dameski, kama baba yangu alivyofanya kule Samaria.”
Ahabu akasema, “Kwa makubaliano, nitakuacha huru.” Hivyo, akaweka mkataba naye, kisha akamruhusu aende zake.
Nabii amlaumu Ahabu
35 Kwa neno la Mwenyezi Mungu, mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake, “Nipige kwa silaha yako,” lakini yule mtu akakataa.
36 Kwa hiyo yule nabii akasema, “Kwa sababu hukumtii Mwenyezi Mungu, mara tu tutakapoachana utauawa na simba.” Na baada ya yule mtu kuondoka, simba akatokea na kumuua.
37 Nabii akamkuta mtu mwingine na kumwambia, “Nipige, tafadhali!” Kisha yule mtu akampiga na kumjeruhi. 38 Ndipo nabii akaenda na kusimama barabarani akimsubiri mfalme. Akajibadilisha kwa kushusha kitambaa cha kichwani mwake hadi kwenye macho. 39 Mfalme alipopita pale, yule nabii akamwita, “Mtumishi wako alienda vitani mahali vilikuwa kali. Mtu mmoja akanijia akiwa na mateka, akasema, ‘Mlinde mtu huyu. Akitoroka, itakuwa uhai wako kwa uhai wake, ama utalipa talanta ya fedha*Talanta moja ni sawa na kilo 34..’ 40 Mtumishi wako alipokuwa na shughuli nyingi hapa na pale, yule mtu akatoweka.”
Mfalme wa Israeli akasema, “Hiyo ndiyo hukumu yako. Wewe umeitaja mwenyewe.”
41 Kisha yule nabii akajifunua macho yake haraka, na mfalme wa Israeli akamtambua kama mmoja wa manabii. 42 Akamwambia mfalme, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Umemwacha huru mtu niliyekusudia afe. Kwa hivyo ni uhai wako kwa uhai wake, watu wako kwa watu wake.’ ” 43 Kwa uchungu na hasira, mfalme wa Israeli akaenda kwenye jumba lake huko Samaria.

*20:39 Talanta moja ni sawa na kilo 34.