4
Kuishi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
1 Kwa hiyo, kwa kuwa Al-Masihi aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia hiyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. 2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki hapa duniani ili kutimiza tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi ili kutimiza mapenzi ya Mungu. 3 Kwa maana wakati uliopita, mmetumia muda mwingi mkifanya yale wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu. 4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika maisha yao ya uovu uliopita kiasi, nao huwatukana ninyi. 5 Lakini itawapasa wao kutoa maelezo kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. 6 Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi kulingana na Mungu aishivyo.
7 Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo kuweni na tahadhari, mkiwa na akili tulivu na kujidhibiti, mkikesha katika kuomba. 8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manung’uniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. 11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote anayehudumu hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kupitia kwa Isa Al-Masihi. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.
Kuteseka kwa kuwa Mfuasi wa Al-Masihi
12 Wapendwa, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata. 13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Al-Masihi, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14 Mkitukanwa kwa ajili ya jina la Al-Masihi, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu. 15 Lakini asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni muuaji, au mwizi, au mhalifu wa aina yoyote, au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine. 16 Lakini ukiteseka kwa kuwa mfuasi wa Al-Masihi, usihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali mtukuze Mungu kwa sababu umeitwa kwa jina hilo. 17 Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje? 18 Basi,
“Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka,
itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu na mwenye dhambi?”
19 Kwa hiyo, wale wanaoteswa kulingana na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.