5
Kulichunga kundi la Mwenyezi Mungu
Kwa wazee walio miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Al-Masihi, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa: lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi. Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji la utukufu lisiloharibika.
Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote jivikeni unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,
“Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye anajishughulisha sana na mambo yenu.
Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.
10 Nanyi baada ya kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Al-Masihi, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.
 
Salamu za mwisho
12 Kwa msaada wa Silvano*yaani Sila, ninayemhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo, na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.
 
13 Kundi la waumini lililoko Babeli, lililochaguliwa pamoja nanyi, wanawasalimu; vivyo hivyo mwanangu Marko anawasalimu.
14 Salimianeni kwa busu la upendo.
 
Amani iwe nanyi nyote mlio katika Al-Masihi.

*5:12 yaani Sila