2 Petro
1
Salamu
1 Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Isa Al-Masihi.
Kwa wale ambao kupitia kwa haki ya Mungu na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu.
2 Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Isa Bwana wetu.
Wito wa Mfuasi wa Al-Masihi na uteule
3 Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 4 Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.
5 Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa; 6 katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa; 7 katika utauwa, upendano wa kindugu; na katika upendano wa kindugu, upendo. 8 Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yatawasaidia kutokosa bidii wala kutokuzaa matunda katika kumjua Bwana wetu Isa Al-Masihi. 9 Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya, haoni mbali na ni kipofu, naye amesahau kwamba ametakaswa kutoka dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe, 11 na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi.
Unabii wa Maandiko
12 Hivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na mmethibitishwa katika kweli mliyo nayo. 13 Naona ni vyema kuwakumbusha mambo haya wakati wote niko katika hema hili ambalo ni mwili wangu, 14 kwa sababu najua kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Isa Al-Masihi alivyoliweka wazi kwangu. 15 Nami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote.
16 Tulipowafahamisha kuhusu uweza na kuja kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake. 17 Alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba*Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana.” 18 Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu.
19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama nuru inavyong’aa gizani, hadi kupambazuke na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu. 20 Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. 21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu wa Mungu.
*1:17 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.