7
Kisha wanaume wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku la Mwenyezi Mungu. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu kilimani, na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku la Mwenyezi Mungu.
Sanduku la Mwenyezi Mungu lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, jumla ya miaka ishirini.
Samweli awatiisha Wafilisti huko Mispa
Nao watu wote wa Israeli wakamrudia Mwenyezi Mungu. Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudia Mwenyezi Mungu kwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi, na kujitoa wenyewe kwa Mwenyezi Mungu na kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi kutoka kwa mkono wa Wafilisti.” Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi yao, nao wakamtumikia Mwenyezi Mungu peke yake.
Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea kwa Mwenyezi Mungu.” Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Mwenyezi Mungu. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.” Naye Samweli alikuwa kiongozi*yaani mwamuzi wa Israeli huko Mispa.
Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti. Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.” Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu. Akamlilia Mwenyezi Mungu kwa niaba ya Israeli, naye Mwenyezi Mungu akamjibu.
10 Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile Mwenyezi Mungu alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli. 11 Wanaume wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari.
12 Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezerimaana yake Jiwe la usaidizi, akisema, “Hadi sasa Mwenyezi Mungu ametusaidia.” 13 Basi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena.
Katika maisha yote ya Samweli, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa dhidi ya Wafilisti. 14 Miji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawa na amani kati ya Israeli na Waamori.
15 Samweli akaendelea kuwa mwamuzi wa Israeli siku zote za maisha yake. 16 Mwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli hadi Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote. 17 Lakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani mwake, huko pia aliamua Israeli. Naye huko alimjengea Mwenyezi Mungu madhabahu.

*7:6 yaani mwamuzi

7:12 maana yake Jiwe la usaidizi