8
Israeli waomba mfalme
Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli. Mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba. Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki.
Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama. Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.”
Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwomba Mwenyezi Mungu. Naye Mwenyezi Mungu akamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao. Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri hadi siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe. Sasa wasikilize, lakini waonye sana, na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.”
10 Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote ya Mwenyezi Mungu. 11 Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake. 12 Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake ya vita. 13 Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji. 14 Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake. 15 Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake. 16 Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ng’ombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe. 17 Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. 18 Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, naye Mwenyezi Mungu hatawajibu.”
19 Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala. 20 Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.”
21 Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele za Mwenyezi Mungu. 22 Mwenyezi Mungu akamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.”
Kisha Samweli akawaambia Waisraeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.”