23
Daudi aokoa Keila
Daudi alipoambiwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila, nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,” akauliza kwa Mwenyezi Mungu, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?”
Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.”
Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Je, si zaidi tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!”
Daudi akauliza kwa Mwenyezi Mungu tena, naye Mwenyezi Mungu akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.” Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila. Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kizibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila.
Sauli amfuata Daudi
Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa ameenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.” Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi.
Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kizibau.” 10 Daudi akasema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu. 11 Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.”
Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, atashuka.”
12 Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?”
Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.”
13 Basi Daudi na watu wake wapatao mia sita wakaondoka Keila, wakawa wanaenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakuenda huko.
14 Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mkononi mwake.
15 Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue. 16 Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu. 17 Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.” 18 Wote wawili wakafanya agano mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi.
19 Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini mwa Yeshimoni? 20 Sasa, ee mfalme, uteremke wakati wowote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.”
21 Sauli akajibu, “Mwenyezi Mungu awabariki kwa kunifikiria. 22 Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali Daudi huenda mara kwa mara, na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mjanja sana. 23 Jueni kila mahali anapojificha, kisha mrudi na kunipa taarifa kamili. Nami nitaenda pamoja nanyi; kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.”
24 Basi wakaondoka na kwenda hadi Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini mwa Yeshimoni. 25 Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akateremka hadi mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi.
26 Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake, 27 mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanaishambulia nchi.” 28 Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamalekothi*maana yake Mwamba wa Kutengana. 29 Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi.

*23:28 maana yake Mwamba wa Kutengana