24
Daudi amwacha Sauli hai
1 Baada ya Sauli kurudi kuwafuatia Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika Jangwa la En-Gedi.” 2 Basi Sauli akachukua vijana wenye uwezo elfu tatu kutoka Israeli yote kwenda kumtafuta Daudi na watu wake karibu na Majabali ya Mbuzi-Mwitu.
3 Akaja kwenye mazizi ya kondoo kando ya njia, hapo palikuwa na pango, na Sauli akaingia ndani kujipumzisha. Daudi na watu wake walikuwa wamo mle pangoni kwa ndani zaidi. 4 Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena Mwenyezi Mungu akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’ ” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli.
5 Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli. 6 Akawaambia watu wake, “Mwenyezi Mungu na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.” 7 Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake.
8 Ndipo Daudi naye akatoka pangoni na kumwita Sauli akisema, “Mfalme, bwana wangu!” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama na kumsujudia, uso wake ukigusa chini. 9 Akamwambia Sauli, “Kwa nini unasikiliza wakati watu wanapokuambia, ‘Daudi amenuia kukudhuru’? 10 Leo umeona kwa macho yako mwenyewe jinsi Mwenyezi Mungu alivyokutia mikononi mwangu huko pangoni. Watu wengine walisisitiza nikuue, lakini nilikuacha, nikisema, ‘Sitainua mkono wangu dhidi ya bwana wangu, kwa sababu yeye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.’ 11 Tazama, baba yangu, ona kipande hiki cha joho lako mkononi mwangu! Nilikata upindo wa joho lako lakini sikukuua. Basi ujue na kutambua kuwa sina hatia ya kutenda mabaya wala kuasi. Wewe sijakukosea, lakini wewe unaniwinda mimi ili kuniua. 12 Mwenyezi Mungu na ahukumu kati yangu na wewe. Naye Mwenyezi Mungu alipize mabaya unayonitendea, lakini mkono wangu hautakugusa. 13 Kama msemo wa kale usemavyo, ‘Kutoka kwa watenda maovu hutoka matendo maovu,’ kwa hiyo mkono wangu hautakugusa wewe.
14 “Je, mfalme wa Israeli ametoka dhidi ya nani? Ni nani unayemfuatia? Je, ni mbwa mfu? Ni kiroboto? 15 Mwenyezi Mungu na awe mwamuzi wetu, yeye na aamue kati yetu. Yeye na anitetee shauri langu; anihesabie haki kwa kuniokoa mkononi mwako.”
16 Daudi alipomaliza kusema haya, Sauli akamuuliza, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Ndipo Sauli akalia kwa sauti kuu. 17 Akamwambia Daudi, “Wewe ni mwenye haki kuliko mimi; umenitendea mema, lakini mimi nimekutendea mabaya. 18 Sasa umeniambia kuhusu mema uliyonitendea. Mwenyezi Mungu alinitia mikononi mwako, lakini wewe hukuniua. 19 Je, mtu ampatapo adui yake, humwacha aende zake bila kumdhuru? Mwenyezi Mungu na akulipe mema kwa jinsi ulivyonitenda leo. 20 Ninajua kwamba hakika utakuwa mfalme na kwamba ufalme wa Israeli utakuwa imara mikononi mwako. 21 Sasa niapie kwa Mwenyezi Mungu kwamba hutakatilia mbali uzao wangu wala kulifuta jina langu kutoka jamaa ya baba yangu.”
22 Basi Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akarudi zake nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.