2
Huduma ya Paulo huko Thesalonike
Ndugu zangu, kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua kwamba kuja kwetu kwenu hakukuwa bure, kama vile mjuavyo, tulikuwa tumeteswa na kutukanwa huko Filipi, lakini hata hivyo, kwa msaada wa Mungu wetu, tulikuwa na ujasiri wa kuwaambia Injili ya Mungu ingawa kulikuwa na upinzani mkubwa. Kwa maana himizo letu halikutokana na hila wala nia mbaya au udanganyifu. Kinyume chake, tulinena kama watu tuliokubaliwa na Mungu tukakabidhiwa Injili. Sisi hatujaribu kuwapendeza wanadamu bali kumpendeza Mungu, yeye ayachunguzaye mawazo ya ndani sana ya mioyo yetu. Kama mnavyojua, hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli ili kuficha tamaa mbaya; Mungu ndiye shahidi yetu. Hatukuwa tukitafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine yeyote, ingawa kama mitume wa Al-Masihi tungeweza kuwa mzigo kwenu. Lakini tulikuwa wapole kati yenu, kama vile mama anawatunza watoto wake wadogo. Tuliwapenda sana, kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu. Ndugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote tulipokuwa tukiwahubiria Injili ya Mungu.
10 Ninyi wenyewe ni mashahidi na Mungu pia, jinsi tulivyokuwa watakatifu, wenye haki na wasio na lawama miongoni mwenu ninyi mlioamini. 11 Maana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake. 12 Tuliwatia moyo, tukiwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yanayompendeza Mungu, anayewaita katika ufalme wake na utukufu wake.
13 Nasi pia tunamshukuru Mungu bila kukoma kwa sababu mlipolipokea neno la Mungu mlilosikia kutoka kwetu, hamkulipokea kama neno la wanadamu, bali mlilipokea kama lilivyo hasa, neno la Mungu, linalotenda kazi ndani yenu ninyi mnaoamini. 14 Kwa maana ninyi ndugu zetu, mlifanyika wafuasi wa makundi ya waumini wa Mungu walio ndani ya Al-Masihi Isa katika Yudea. Mlipata mateso yale yale kutoka kwa watu wenu wenyewe kama vile waumini hao walivyoteswa na Wayahudi, 15 wale waliomuua Bwana Isa na manabii, nasi wakatufukuza pia. Watu hao walimchukiza Mungu na tena ni adui wa watu wote, 16 wakijitahidi kutuzuia tusizungumze na watu wa Mataifa ili wapate kuokolewa. Kwa njia hii wanazidi kujilundikia dhambi zao hadi kikomo. Lakini hatimaye ghadhabu ya Mungu imewafikia.
Paulo atamani kuwaona Wathesalonike
17 Lakini ndugu zetu, tulipotenganishwa nanyi kwa muda mfupi (ingawa kutengana huko kulikuwa kwa mwili tu, si kwa moyo), tulizidi kuwa na shauku kubwa kuwaona uso kwa uso. 18 Maana tulitaka kuja kwenu, hasa mimi Paulo, nilitaka kuja tena na tena, lakini Shetani akatuzuia. 19 Kwa maana tumaini letu ni nini, au furaha yetu, au taji letu la kujisifia mbele za Bwana wetu Isa Al-Masihi wakati wa kuja kwake? Je, si ni ninyi? 20 Naam, ninyi ndio fahari yetu na furaha yetu.