1 Wathesalonike
1
Salamu
Paulo, Silvano*yaani Sila na Timotheo.
Kwa kundi la waumini la Wathesalonike, ninyi mlio ndani ya Mungu, BabaKwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, na ndani ya Bwana wetu Isa Al-Masihi.
Neema iwe kwenu na amani.
Shukrani kwa ajili ya imani ya Wathesalonike
Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima. Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Isa Al-Masihi.
Ndugu zetu mnaopendwa na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua, kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho wa Mungu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda kati yenu kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana Isa, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho wa Mungu. Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya. Kwa maana kutoka kwenu neno la Bwana Isa limesikika, si katika Makedonia na Akaya tu, bali pia imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali, kiasi kwamba hatuna haja ya kusema chochote juu yake. Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli, 10 na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu: yaani Isa, yeye aliyetuokoa kutoka ghadhabu inayokuja.

*1:1 yaani Sila

1:1 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.