4
Ninyi mabwana, watendeeni watumwa wenu yaliyo haki na yanayostahili, mkitambua kwamba ninyi pia mnaye Bwana mbinguni.
Maagizo zaidi
Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru. Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena neno lake, ili tupate kuitangaza siri ya Al-Masihi, ambayo kwa ajili yake nimefungwa. Ombeni ili nipate kuitangaza hiyo siri kwa udhahiri kama inipasavyo. Nendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.
 
Salamu za mwisho
Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtendakazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana Isa. Nimemtuma kwenu kwa lengo maalum la kuwafahamisha hali yetu, na pia awatie moyo. Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu.
 
10 Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni.) 11 Isa aitwaye Yusto pia anawasalimu. Hawa peke yao ndio Wayahudi miongoni mwa watendakazi wenzangu kwa ajili ya ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu.
12 Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Al-Masihi Isa, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu, mkiwa wakamilifu na thabiti. 13 Ninashuhudia kumhusu kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli.
14 Rafiki yetu mpendwa, Luka yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu.
15 Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia, na pia Nimfa, pamoja na kundi la waumini wanaokutana katika nyumba yake.
 
16 Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kundi la waumini wa Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia.
 
17 Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana Isa.”
 
18 Mimi Paulo naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi.