3
Kanuni za kuishi maisha matakatifu
Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Al-Masihi, yatafuteni yaliyo juu, Al-Masihi alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Al-Masihi katika Mungu. Al-Masihi, aliye uzima wenu, atakapofunuliwa, ndipo nanyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.
Basi, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambao ni ibada ya sanamu. Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo. Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Al-Masihi ni yote, na ndani ya yote.
12 Basi, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wanaopendwa sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana Isa alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
15 Amani ya Al-Masihi na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Al-Masihi na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Isa, mkimshukuru Mungu Baba*Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi kupitia kwake.
Kanuni katika madaraka ya nyumbani
18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana Isa.
19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe wakali kwao.
20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hii inampendeza Bwana Isa.
21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.
22 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, wala si kwa kujipendekeza tu kwao, bali kwa moyo mnyofu na kumcha Bwana. 23 Lolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo wote kama watu wanaomtumikia Bwana Isa, na si wanadamu, 24 kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Isa Al-Masihi mnayemtumikia. 25 Yeyote atendaye mabaya atapewa adhabu ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.

*3:17 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.